Rais wa Marekani Joe Biden, amemshtumu Rais wa Urusi Vladimir Putin kupanga kutumia silaha za kemikali dhidi ya watu wa Ukraine, baada ya kudai kuwa Kiev ina hifadhi ya silaha hizo hatari.
Aidha, kiongozi huyo wa Marekani amewaambia wamiliki wa kampuni wawe makini, kwa sababu Urusi inapanga kutekeleza mashambulizi ya mtandao.
"Kiwango cha Urusi kutekeleza uvamizi wa kimtandao, hauwezi kupuuzwa, na hii inakuja, idara ya serikali inajiandaa kuhusu hili, na ushauri wangu ni kuwa, kwa nyie mashirika ya kibinafasi kuhakikisha kuwa biashara zenu zinaletwa kwa kutumia sheria zetu, lajkini acha niseme kitu kimoja, hili sio suala la biashara tu lakini lina maslahi mapana ya kitaifa."
Katika ujumbe wa video alioutoa Jumatatu, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewataka Waukraine kufanya kila liwezekanalo kuilinda nchi na serikali yao. Amewaita wanajeshi wa Urusi "wavamizi" wanaostahili kufukuzwa nje ya taifa hilo ili raia wa Ukraine waishi pamoja na kwa amani.
Zelensky amewataja wanajeshi wa Urusi kama "watalii wenye silaha" na "watumwa wa propaganda" ambazo zimebadilisha ufahamu wao. Kiongozi huyo wa Ukraine amesema nchi yake itaangamizwa kabla ya kusalimisha miji yake kwa wanajeshi wa Urusi.