AU yakemea unyanyasaji wa Waafrika maeneo ya mpaka wa Ukraine
Umoja wa Afrika umepinga unyanyasaji wa Waafrika wanaojaribu kutoka Ukraine na kuvuka kuelekea katika nchi jirani.
Taarifa kutoka umoja wa bara hilo ilisema mapema Jumatatu kwamba Waafrika wakitengwa kutakuwa na ubaguzi wa rangi na ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Iliongeza kuwa watu wote wana haki sawa ya kuvuka mipaka ya kimataifa kutokana na migogoro, bila kujali utaifa wao au utambulisho wa rangi.
Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine wiki iliyopita, Waafrika na watu wengine wa rangi mbalimbali wameripoti kutendewa vibaya na maafisa wa mpaka wa Ukraine, huku baadhi wakidai kuwa walizuiliwa kupanda treni na mabasi yanayokimbia miji wakishambuliwa au waliambiwa tu wasubiri kwenye maeneo ya mpakani huku wengine waliruhusiwa.
Baadhi ya wanafunzi wa Kiafrika waliripoti kuzuiwa kuingia hotelini na kulala barabarani.