Wizara ya Afya imepongeza wadau na wafadhili mbalimbali wanaondelea kufadhili miradi mbalimbali ya afya, ukiwemo mradi wa mafunzo ya epidemiolojia kwa vitendo (field epidemiology) kwa wanafunzi wa afya, katika kuwajengea uwezo na ujuzi katika taaluma ya Afya.

Hayo yamesemwa na Dkt. Witness Mchwampaka, wakati akifungua mkutano wa wataalamu wa Afya wanaohusika na usimamizi wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaokwenda maeneo mbalimbali kujifunza kwa vitendo pamoja na kujengewa uwezo baada ya mafunzo ya darasani.

Amesema..”Wizara kupitia kitengo cha Epidemiolojia kinatambua mchango mkubwa wa wataalamu waafya katika kusimamia wanafunzi wanaopangiwa kufanya mafunzo kwa vitendo maeneo mbalimbalikatika ngazi za Taifa, Mkoa na Wilaya nchini na kwamba matokeo makubwa ya kazi nzuri inayoendeleakufanywa na wasimamizi hao katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa mradi huo mwaka 2008, ni umahiriwa wanafunzi wa afya wanaohitimu hususani katika maeneo ya ukusanyaji wa taarifa, utafiti na tathmini
ya mifumo ya Afya.

Amewataka wataalamu hao waliokutana kwa siku moja kujadili mafanikio, changamoto, uzoefu naushauri katika usimamizi kati ya wanafunzi na wasimamizi wanapokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo,pamoja na kuendelea kuwapa ushirikiano wanafunzi na kuwajumuisha katika masuala mbalimbali ya kiutafiti na uchambuzi wa taarifa ili kupitia wanafunzi hao, Taifa liweze kupata wataalamu bora na wabobevu katika uchambuzi wa mifumo na utafiti ili elimu ya darasani iendane na vitendo.

Mkutano huu wa mwaka “National Supervisors Workshop” unakutanisha wataalamu kutoka Sekta mbalimbali za Afya, na umelenga kufanya tathmini ya jumla ya mwenendo wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, changamoto, motisha na kupendekeza mbinu mpya za usimamizi wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Epidemiolojia kwa vitendo.

Naye Mratibu wa mradi huo Dkt. Rogath Kishimba, amechanganua mafanikio mbalimbali ambayo Serikali imeendelea kuyapata kupitia mradi wa mafunzo kwa vitendo unaofanywa kwa ushirikiano na Chuo cha Afya cha Muhimbili, na kuanisha taratibu na sifa zinazotumika kuainisha maeneo ya vitendo kwa mafunzo, pamoja na mipango mbalimbali ambayo Serikali kupitia Wizara ya Afya na wafadhili imelenga kuendelea kufanya kama sehemu ya maboresho, ili wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo kunufaika na mpango huo.

Washiriki wa Mkutano huo wametoka katika Programu ya kuzuia maambukizi ya VVU, Mpango wa Taifa wa Udhibiti wa Malaria,Afya ya Mazingira, Kitengo cha Taifa cha Kinga, Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto, Programu ya Seli Mundu, Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD), Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Maabara ya Taifa, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu Mzumbe. Mkutano huo umefadhiliwa na Serikali ya Watu wa Marekani kupitia mradi wa Kituo cha Udhibiti maradhi (CDC) unaotekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe.