Serikali imetoa maelezo kuhusiana na kuwapo kwa malalamiko ya wizi wa ‘bandle’ la simu. Maelezo hayo yametolewa na Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari, Nape Nnauye bungeni.

Nape alisema kwamba kutokana na malalamiko ya watumiaji wa ‘bandle la simu, serikali ilifanya tathmini, ambayo imebainisha kwamba hayana ukweli, bali zinakwisha kutokana na simu za kisasa wanazotumia watu.

Akijibu hoja mbalimbali za wabunge na kamati ambao wamelalamika kwa wizi wa bandle, Nape , alisema uwezo wa Mamlaka ya Mawasilinao Tanzania (TCRA), kufuatilia miamlaka mbalimbali umeongezeka.

“Tunaendelea kuchambua taarifa mbalimbali juu ya mamalamiko ya matumizi ya bandle kwenye simu zetu, hoja kwamba kuna zinazowekwa zinatumika bila mtumiaji kuzitumia, yamekuwapo malalamiko yamefikishwa kwenye mamlaka husika na uchambuzi umefanyika,” alisema na kuongeza:

“Matokeo ya uchambuzi yanaonyesha hakuna wizi uliotokea isipokuwa kuna tatizo la matumizi ya simu za kisasa, yamejikita kwenye simu za kisasa baadhi ya ‘application’ zinatumia ‘bandle’ bila mwenye simu kujua, nyingine simu hizo unaweza kuweka bandle na kuwasha ‘data’ kupitia ‘hot sport; ambayo inatumiwa na mtu mwingine.”

“Kuna watu wamechunguzwa ikabainika kuna watu wametumia bandle zao.”

Alisema suluhisho lililoletwa ni kupitia Baraza la Watumiaji wa Huduma za Simu ambao wametengeneza ‘application’ ya mtumiaji wa simu kufuatilia matumizi yake na ataweza kuzima baadhi ya ‘application’ zinazotumia mtandao wake.

“Tunafanya majaribio ya ‘application hiyo na itakapokuwa tayari watumiaji watapewa na kufuatilia. Pia tunatoa elimu ya matumizi ya simu za kisasa ili watu wasiingie kwenye gharama kwa kutokujua,” alisema Nape.

Aidha, alisema utafiti umeonyesha shida kubwa ni kwenye matumizi badala ya wizi na kwamba hadi sasa hawajakamata wizi wowote.

“Jambo hili limekuwa kubwa na linazungumzwa muda mrefu, ni rahisi kudhani kuna wizi na tukawahukumu watoa huduma lakini TCRA, malalamiko yoyote hakuna lalamiko limethibitisha kuna wizi, bado yanaendelea kupokelewa,”alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, alisema wanaishauri serikali iisimamie TCRA kukutana na wadau na watoa huduma, ili kuona chanzo cha kupungua kwa miamala ya simu kwa lengo la kutatua changamoto hizo.

“Kamati ilibaini kupungua kwa miamala ya simu, jambo linalokinzana na matarajio ya kisera katika sekta. Kupungua kwa miamala hiyo ya simu ni ishara ya changamoto ya shughuli za umma za udhibiti na uendeshaji wa sekta ya mawasiliano, hali inayohitaji kurekebishwa mapema,”alisema.