Waziri Mkuu Azungumza Na Wabunge Wa Bunge La Marekani.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Nchi ya Marekani katika sekta zote za maendeleo ili kusaidia kuongeza fursa za uwekezaji na biashara.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Februari 23, 2022) alipozungumza na wabunge wa Bunge la Marekani Katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu amesema kuwa wabunge hao wamefurahi kuona mahusiano kati ya nchi hizi mbili yanakua.
“Mahusiano yetu kiuchumi yanaendelea kuimarika, wanatambua mchango wa Tanzania katika kutoa fursa za uwekezaji hapa Tanzania na sisi kufanya nao biashara, tutaendelea kuimarisha kwa kuwa na ‘forum’ mbalimbali za wafanyabishara wa ndani ya Nchi na Wamarekani.”
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuifungua Tanzania kimataifa katika maeneo mbalimbali ili kuongeza fursa kwa Watanzania.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza tufanye mapitio na maboresho ya uwekezji na biashara, kwa kupitia sheria zetu na kuondoa maeneo ambayo yanakwaza wafanyabishara na kujenga uwezo kwa Watanzania kufanya biashara nje ya nchi, lengo ni kuinua uchumi na kufungua fursa za ajira kwa vijana wetu”
Amesema kuwa wabunge hao wameahidi kushirikiana na Tanzania katika mpango wa kuinua uchumi katika meneo mbalimbali kupitia miradi na programu mbalimbali kupitia taasisi za kimarekani.
“Wameahidi kuendelea kuwa nasi na sisi tumeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu, tutaendelea kumpa ushirikiano balozi wa Marekani ili tuweze kuongeza fursa za mashirikiano katika maeneo mengi zaidi na misaada yote tutaitumia katika malengo yaliyokusudiwa”
Mheshimiwa Majaliwa amewataka wabunge hao kuwa mabalozi wa kuhamasisha utalii kati ya Tanzania na Marekani kwa kuwa Tanzania imebarikiwa vivutio vingi “eneo la utalii tumewahamasisha ndugu zetu waje kuona vivutio vingi tulivyonavyo”
Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa wabunge hao kujenga uhusiano wa Kibunge kati ya bunge la Marekani na bunge la Tanzania “Lengo ni wabunge hawa wapate nafasi ya kutembeleana na kubadilishana mawazo ya namna bora ya kuendesha mabunge yetu”
Mheshimiwa Majaliwa amesema amewaeleza wabunge hao kuwa Tanzania inaendelea kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi “tumewaambia pia Tanzania tunahitaji ‘support’ kwa mataifa yanayoshughulikia mabadiliko ya tabianchi na wameahidi kutuunga mkono kwenye eneo hili”.
Wabunge walioshiriki mkutano huo ni Gregrory Meeks, Ami Bera, Ilhan Omar, Joyce Beatty, G.K Butter, Brenda Lawrence na Troy Carter. Wabunge hao waliambatana na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Dk. Donald Wright