WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameunda timu maalum ya watu tisa ambayo imepewa jukumu la kuchunguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi, Tanga.

“Kamati hiyo inapaswa kuanza kazi yake kesho(leo) na inatakiwa iwe imekamilisha ripoti yake ndani ya siku 14,” amesema Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa jana (Ijumaa, Februari 4, 2022) mjini Magu, Mwanza akiwa njiani kuelekea Musoma, Mara kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya CCM.

Mheshimiwa Rais amesema anatambua Jeshi la Polisi limeunda kamati ya uchunguzi lakini ameagiza iundwe kamati hiyo huru ili ikafanye uchunguzi wa mauaji ya Mtwara yaliyofanywa na askari polisi. Mauaji ya Mtwara yalitokea Januari 05, 2022 na mauaji ya Kilindi yaliyotokea Januari 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kamati hiyo ina maafisa wenye dhamana kutoka mamlaka tofauti za Serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, TAKUKURU, Ofisi ya Mwanansheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro awasimamishe kazi maafisa wa Polisi wa Mtwara na Kilindi ili kupisha uchunguzi wakati timu aliyoiunda ikifanya kazi yake.

“Viongozi hawa wanapaswa wakae pembeni, watahojiwa na hii timu wakiwa nje ya ofisi,” amesema Waziri Mkuu na kuwataja maafisa hao kuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara (RPC), Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mtwara (RCO) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara cha eneo alilofia mfanyabiashara Mussa Hamisi Hamisi na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Greyson Mahenge anayedaiwa kujinyonga.

Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kilindi na Afisa Upelelezi wa Wilaya nao pia wakae pembeni kupisha uchunguzi.