Waziri Mkuu apokea taarifa ya Mauaji ya Mtwara na Kilindi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya kamati maalum aliyoiunda kwa ajili ya kuchunguza mauaji katika Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Kilindi, Tanga.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu ameipongeza kamati hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya na kwa umakini mkubwa.
“Taarifa hii imeeleza kila kitu bayana kabisa, na haya ndio matarajio ya Serikali yetu kwamba mtumishi yeyote ndani ya Serikali lazima awajibike kwa weledi, uaminifu na uadilifu mkubwa, kwa kufanya hivyo shughuli za kuwahudumia wananchi zitakwenda vizuri sana”
Amesema kuwa baada ya kuipitia taarifa hiyo ataiwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyetoa maagizo ya kuundwa kwa kamati hiyo ya kuchunguza mauaji kwenye Mikoa ya Mtwara na Tanga.
“Rais Samia anahitaji kuona matokeo, tena matokeo yasiyomuonea mtu yeyote, lakini matokeo yatakayomuwajibisha yeyote ambaye atagundulika kuhusika kutaka kuleta tafrani ndani ya nchi”
Kamati hiyo ilianza kazi Februari 4, 2022 ilipaswa kukamilisha ripoti yake ndani ya siku 14, zilizoishia Februari 17, 2022, lakini kutokana na ukubwa wa kazi na mahitaji ya kujiridhisha na baadhi ya masuala, kamati iliomba kuongezewa siku saba kuanzia Februari 17 hadi Februari 23, 2022.
Kamati hiyo iliundwa na Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Februari 4, 2022 Wilayani Magu, Mwanza akiwa njiani kuelekea Musoma, Mara kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya CCM.