WATU 74 wamefariki dunia Mkoa wa Geita kwa kujinyonga, wivu wa mapenzi na wizi kwa miezi minane kuanzia Juni mwaka 2021 hadi Januari mwaka huu.

Hayo yalibainishwa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe, alipozungumza na viongozi wa dini katika Halmashauri ya Mji wa Geita.

Mwaibambe, alisema watu hao walikufa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, na kwamba kuanzia Agosti mwaka 2021 hadi Januari mwaka huu, watu 46 walifariki dunia kwa sababu mbalimbali, kati yao wawili walikufa kwa imani za kishirikina, 10 kwa wivu wa mapenzi, wanane walikufa kwa ugomvi wa kawaida, watatu kwa uhalifu na 23 kwa wizi.

Alisema kati ya Juni mwaka 2021 hadi Januari mwaka huu, watu 28 walikufa kwa kujinyonga katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita, hivyo kusababisha taharuki kwa wananchi wa mkoa huo.

Kamanda Mwaibambe aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha wanawaeleza waumini wao kuhusiana na matukio hayo na kuwahubiria maadili mema ili kukomesha matukio hayo ya kujinyonga na uhalifu katika Mkoa wa Geita.