WATOTO wawili wa familia moja wamefariki dunia baada ya kukosa hewa ya kutosha chumbani katika nyumba waliyokuwa wakiishi katika Kijiji cha Usubilo kata ya Ifucha, halmashauri ya manispaa Tabora.  

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kutaja watoto waliofariki kuwa ni Amani Athuman (1 ½ ) na Zainabu Athumani (1).

Alisema kuwa tukio hilo limetokea Februari 5 mwaka huu majira ya saa 6.30 usiku chanzo kikiwa ni moto uliokuwa umewashwa ndani ili kuwapa joto watoto hao kutokana na baridi kali kipindi hiki cha mvua.

Alieleza kuwa moshi wa moto huo ulipelekea watoto hao waliokuwa wamelala kukosa hewa ya kutosha kutokana na miundombinu midogo ya kupitisha hewa katika nyumba hiyo.

Alibainisha kuwa miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu ili taratibu zingine za mazishi ziendelee.

Kamanda alitaja wahanga wengine katika tukio hilo kuwa ni baba mzazi wa watoto hao Athuman Shaban (45) Mnyamwezi, mkulima, mkewe Magreth Joseph (34) Msukuma, mkulima na binti yao Neema Athumani (17) wote ni wakazi wa Ifucha.

Alibainisha kuwa wahanga wote wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo (Kitete) kwa ajili ya matibabu zaidi na hali zao hadi sasa bado hazijaimarika vizuri.

Alitoa wito kwa jamii kuangalia usalama wa watoto wao hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zinaendelea kunyesha kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo ili wasidhurike.