Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Zanzibar
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) hadi kufikia 31 Januari, 2022, imesajili jumla ya wananchi wa Zanzibar wenye sifa stahiki   806,197  sawa na asilimia 88% ya lengo la kusajili watu 919,117 ifikapo Machi 2022 na hivyo kufanya jumla ya Watanzania waliosajiliwa kufikia  22,802,296 Bara na Zanzibar mpaka tarehe 31 Januari 2022.

Akizungumza  Februari 13, 2022 Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Gerson Msigwa akiwa Visiwani Zanzibar, wakati akitoa taarifa ya wiki kuhusu utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo mbalimbali nchini.

 Msigwa alisema “jumla ya vitambulisho 731,079 vimezalishwa kwa upande wa Zanzibar sawa na asilimia 91% ya vitambulisho vilivyotarajiwa kutolewa kwa watu 806,197 waliosajiliwa.  Kati ya hivyo, Vitambulisho 642,277 vimegawiwa kwa wananchi. Kwa sasa kazi za usajili na utambuzi wa watu zinaendelea kufanika kwa kasi kubwa katika ngazi za Wilaya kwa wananchi wote.”

Aliongeza kuwa idadi hii inafanya jumla ya vitambulisho vya Taifa vilivyozalishwa kwa nchi nzima Tanzania bara na Visiwani kuwa 10,643,154 na Vitambulisho vilivyokwisha kugawiwa kwa wananchi kuwa 9,860,894.

Ili kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, Msigwa anasema kuwa mpaka sasa jumla ya wilaya sita (06) za Zanzibar zimeunganishwa na mtandao wa Mawasiliano na Kituo  cha kuchakata maombi cha Data Centre  kilichoko Kibaha Pwani na hivyo kurahisisha uchakataji wa maombi na uzalishaji wa namba za utambulisho na vitambulisho vya Taifa.

Anataja wilaya hizo kuwa ni ChakeChake Mkoa wa Kusini Pemba, Ngombeni Mkoa wa Kusini Pemba, Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mjini/Unguja Mkoa wa Mjini Magharibi, Magharibi A / Mwanakwerekwe Unguja Mkoa wa Mjini Magharibi na Wilaya ya Kati Dunga Mkoa wa Kusini Unguja.

“Mafanikio haya yametokana na kuwepo kwa Mkongo wa Taifa uliowezesha kufanya maunganisho ya mtandao. Wilaya za Zanzibar zilizounganishwa. Hii inafanya ofisi zilizounganishwa na Kituo cha kituo cha uchakataji taarifa kwa Tanzania Bara na Zanzibar kuwa 130 kati ya Wilaya 150” alisema Msigwa.