Na Englibert Kayombo WAF - Dodoma.
MAMLAKA ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) chini ya Wizara ya Afya imetakiwa kuweka mazingira rafiki ya kuvutia wawekezaji wa kitanzania pamoja na kuondoa vikwazo ambavyo vinaweza kuzorotesha wagunduzi kusajili bidhaa zao nchini.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo Mhe. Kirumbe Ng’enda wakati wa kikao killicholenga kupitia Sheria Ndogo za TMDA kilichohudhuriwa na Viongozi pamoja wataalam kutoka Wizara ya Afya na TMDA wakiongozwa na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel.
Wajumbe wa Kamati hiyo wasemeka kuwa Serikali imekuwa ikitilia mkazo zaidi kwa kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi na kusahau kuwa wapo watanzania pia ambao wanaweza kuwekeza au kuja na ugunduzi ambao utalinufaisha Taifa.
Wajumbe wa Kamati wamesema Sheria ndogo zinazotungwa pia ziwalinde Watanzania na kuweka mazingira rafiki ya kuwavutia wawekezaji wazawa wa hapa nchini na kurahisisha shughuli za usajili wa bidhaa mbalimbali.
Awali akizungumza Naibu Waziri wa Afya Dkt. Mollel amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Shilingi Bilioni 6.1 kwa ajili ya kufanya shughuli za Tafiti mbalimbali ambazo zitaleta tija kwa Taifa.
“Tuanze sasa kuwafadhili wagunduzi wetu wa ndani ya nchi kupitia fedha hizi Bilioni 6.1 alizotupa Rais Samia Suluhu Hassan na tupunguze utegemezi wa mataifa ya nje kuja kutufadhili kufanya tafiti hapa nchini kwetu” amesema Naibu Waziri Dkt. Mollel.
Aidha Dkt. Mollel amesema changamoto wanazopitia wawekezaji na wagunduzi wa bidhaa mbalimbali hapa nchini zimepokelewa na tayari zimeanza kufanyiwa kazi na kuiahidi Kamati hiyo kuwa muda sio mrefu Wizara itakuja na suluhisho.
“Kuna vitu ambavyo Watanzania wanagundua na vina manufaa sana kwa nchini lakini wanakwama kwenye masuala mbalimbali ikiwemo usajili kutokana na ukosefu wa fedha, tunakwenda kuweka mfumo mzuri wa kuwasaidia na tutarudi na majibu mazuri” amesema Dkt. Mollel.