Serikali ya Tanzania imepata msaada wa Euro milioni 425 ambayo ni sawa na shilingi trilioni 1.15 kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EC) kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rais wa Kamisheni hiyo, Mhe. Ursula von der Leyen ametangaza kiasi hicho cha msaada baada ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyeko ziarani nchini Ubelgiji.

Fedha zilizotolewa zinatarajiwa kutumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo nchini Tanzania.

Tanzania imeainisha kutumia Euro milioni 180 sawa na shilingi bilioni 480, kwenye miradi mitatu ikiwemo ya kuimarisha mifumo ya kidijitali kwa gharama ya shilingi bilioni 92.

Eneo lingine ni kuimarisha ustawi wa jamii ya Watanzania kwa kuzingatia usawa wa jinsia ambapo kiasi cha shilingi bilioni 284 zimekusudiwa kwa mradi huo.

Shilingi bilioni 197.3 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miji (Green Cities) ambapo kwa awamu ya kwanza mikoa inayotarajiwa kunufaika ni pamoja na Tanga, Mwanza na Pemba.

Mhe. Von der Leyen amemfahamisha Rais Samia kuwa Tanzania pia ni miongoni mwa nchi za Afrika zitakazonufaika na mpango mpya wa EU (Global Gateway Investment Package) unaokusudia kukabiliana na changamoto ikiwemo ajira na kuimarisha huduma za afya, elimu na uchumi wa buluu.

Rais Samia ameahidi kuendelea kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EC) kuainisha maeneo mengine ya kipaumbele kupitia mashauriano ya pande zote mbili baadaye ili msaada huo ulete ustawi wa maendeleo kwa Watanzania.