Kutoka Dar es Salaam, Februari 18,2022
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya leo Februari 18 imepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi Milioni 578 vitavyosaidia kwenye matibabu katika hospitali za Rufaa za mikoa ya Mwanza, Arusha, Dodoma na Tanga.

Vifaa hivyo ni pamoja na Oxygen cylinders (656), Hand-held gas monitors (20), Pulse oximeters (184), Glucometers (100), Gauge na flowmeters (636) na Oxygen cylinder carts (208) vitavyosaidia kwenye matibabu, hususan katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Akipokea vifaa hivyo Jijini Dar es Salaam kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la “Save the Children” Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe ameelekeza utunzaji mzuri wa vifaa hivyo ili vilete tija kwa Wananchi wanaoenda kupata huduma za matibabu.

“Vifaa hivi ni gharama sana, nitoe wito kwa watakaoenda kuvitumia, kuhakikisha wanavitumia kwa uangalifu mzuri na kuvitunza ikiwemo kuvifanyia uboreshaji ili viweze kuwasaidia wananchi wenye uhitaji wa huduma ” Amesema Dkt. Sichalwe.

Aidha Dkt. Sichalwe amesema kuwa, Serikali imelenga kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini kwa kujenga, kukarabati na kununua vifaa vya idara za dharura (EMD) na Idara za wagonjwa mahututi (ICU) nchi nzima ili kuwasaidia wananchi wenye uhitaji wa huduma hizo.

Ameendelea kusema kuwa, hadi sasa Serikali imefunga mitambo 12 ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni na kufanya jumla mitambo 19 nchi nzima, huku akisisitiza kuwa tayari mitungi ya hewa ya Oksijeni zaidi ya 4600 imesambazwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tunafunga mitambo mingine 12 ya kuzalisha hewatiba ya Oksijeni, kwa fedha za Serikali na kufikisha jumla mitambo 19 nchini na tumekwisha sambaza mitungi ya hewa tiba ya oksijeni zaidi ya 4,600.” Amesema Dkt. Sichalwe.

Sambamba na hilo, amewata “Save the Children ” kushirikiana na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Afya, ili mradi uweze kuwanufaisha wagonjwa bila kuchelewa.

Mbali na hayo Dkt. Sichalwe, amewataka “Save the Children ” kuweka kipaumbele shughuli za uhamasishaji wa wananchi kupata Chanjo ya UVIKO-19 ili kujua umuhimu wa kuchanja kisha wafanye maamuzi ya kwenda kuchanja kwa hiari.

Naye Meneja Uchechemuzi (Advocacy Manager) kutoka Shirika la SavetheChildren Bw. Oscar Kimaro amesema, Shirika la Save the Children litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha utoaji huduma za afya kwa wananchi, hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali inapambana na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19.

Amesema, katika Mikoa hiyo minne ambayo itapata vifaa hivyo lengo ni kuhakikisha wagonjwa wanaofika katika hospitali hizo wanapata huduma bora na kwa haraka kutokana na ubora na ufanisi wa vifaa hivyo.