Serikali yaondoa tozo ya petroli, dizeli, mafuta ya taa
Serikali imeondoa tozo ya Sh100 kwa kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa miezi mitatu kuanzia mwezi Machi.
Taarifa iliyotolewa Jumatatu Februari 28, 2022 na Wizara ya Nishati imesema kuwa sababu za kuondoa tozo hiyo ni kutokana na kuendelea kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia kunakosababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo vita kati ya Urusi na Ukraine.
“Pamoja na kwamba uamuzi huu utaipunguzia Serikali mapato ya kiasi cha Shilingi bilioni 30 kwa mwezi, Serikali imeona ni muhimu kuendelea kuwalinda wananchi wake dhidi ya athari za mabadiliko ya bei za mafuta ulimwenguni. Hii inatokana na ukweli kwamba endapo uamuzi huu usingechukuliwa na Serikali, bei za mafuta nchini kuanzia mwezi Machi na kuendelea zingekuwa za juu sans kutokana na sababu zilizoelezwa hapo juu” imesema taarifa hiyo
Taarifa hiyo imesema kuwa Waziri wa Nishati, January Makamba ameidhinisha na kusaini marekebisho ya kanuni inayohusika na Tozo hiyo ili kutimiza uamuzi huu wa Serikali.