Serikali Yagawa Miche Milioni Mbili Kwa Wakulima Wa Kahawa
Naibu Waziri wa Kilimo Mh Anthony Mavunde amegawa miche 2,000,000 kwa wakulima wa kahawa aina ya robusta iliyozalishwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kupitia Kampuni ya JJAD FARMERS Ltd, zoezi lililofanyika wilayani Kyerwa,Mkoani Kagera kwa lengo la kuhamasisha wakulima wa kahawa kuongeza uzalishaji ili kufikia malengo ya uzalishaji wa Kahawa tani 300,000 ifikapo mwaka 2025.
Akitoa maelezo ya awali,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Bw. Primus Kimaryo amesema Bodi ya Kahawa itaendelea kushirikisha wadau wote katika uzalishaji miche bora ya kahawa kwa kuwa mibuni mingi iliyopo mashambani hivi sasa imezidi miaka 25 na hivyo imepungua uwezo wa uzalishaji wa kahawa.
“Niwapongeze Bodi kwa kuamua kuishirikisha sekta binafsi kuzalisha miche bora ya kahawa.Niipongeze kampuni ya JJAD kwa kuzalisha miche bora ya kahawa kama ambavyo mkataba ulielekeza.
Serikali chini ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wa zao la kahawa sambamba na utafutaji wa masoko ya uhakika ya kahawa ili kumnufaisha mkulima wa Tanzania na ndio maana leo serikali inagawa miche hii milioni mbili kwa wakulima bila gharama yoyote kama kichocheo cha kuwafanya mzalishe kwa wingi zaidi.
Maelekezo yangu kwenu nyote;
-Bodi ya Kahawa Tanzania iweke mikakati madhubuti ya upatikanaji wa soko la uhakika la kahawa kwa bei itakayomnufaisha mkulima.
-Bodi ya Kahawa Tanzania kuhakikisha inafikisha lengo la uzalishaji wa miche bora ya Kahawa 20,000,000 kwa mwaka.
-Malipo ya mazao ya wakulima yafanyike kwa wakati kwa kuendelea kuruhusu ununuzi wa mazao kupitia AMCOS na wanunuzi binafsi.
-Maafisa Ugani kufuatilia upandaji wa miche hii na kuendelea kutoa elimu kuhusu kanuni bora za kilimo cha kahawa . “Alisema Mavunde
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Prof. Aurelia Kamuzora* amesema moja ya jukumu kubwa ambalo wanalitekeleza sasa ni upatikanaji wa masoko ya uhakika ya kahawa na tayari wameanza mazungumzo na makampuni makubwa ya Ulaya juu ya namna bora ya upatikanaji wa soko la kahawa ya Tanzania ambalo ni endelevu na lenye kuzingatia uwazi na pia ubora wa kahawa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mh. Shaibu Mwaimu ametoa onyo kwa watu wanaofanya biashara ya magendo ya kahawa kuacha mara moja na kwamba serikali itawachukulia wote watakaohusika na biashara hiyo ya magendo. Alisema ‘serikali miche inayotolewa ni rasilimali ya serikali’ tuitumie vizuri tuondokane na umasikini.