Na WyEST,Kilimanjaro.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda  amesema Serikali itahakikisha inaweka mgawanyo sawa wa rasilimali za elimu nchi nzima ili kuwezesha watoto wote wa Kitanzania kupata elimu na mazingira bora ya ujifunzaji.
 
Akizungumza katika uzinduzi wa Mradi wa TEHAMA kwa Shule za Sekondari za Serikali uliofanyika katika Shule ya Sekondari Mawenzi Mjini Moshi Waziri huyo amesema kuwa ni lazima watoto wote wa Kitanzania wapate fursa sawa kwenye elimu bila kujali eneo analotoka.
 
“Mgawanyo wa fursa za elimu nchi nzima ni lazima uwe sawa na wa haki ili mtoto asije kukosa fursa nzuri kwa sababu amezaliwa katika Wilaya fulani na mwingine wa Wilaya nyingine anapata fursa nzuri zaidi wakati watoto wote hawa ni Watanzania,” amesema Prof. Mkenda.
 
Profesa Mkenda amesisitiza kuwa Serikali inataka kuona TEHAMA inatumika katika kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu pamoja na kuimarisha ubora wa mafunzo.
 
Waziri Mkenda amesema kuwa  katika kufanikisha hilo Serikali imeendelea kuweka msisitizo katika maeneo ya Sayansi na Teknolojia  ili kuwezesha Watanzania kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ikiwa ni pamoja na kuandaa mitaala ya elimu,  miongozo na kutunga Sera zinazohusu matumizi ya TEHAMA na Teknolojia saidizi.
 
Mhe. Mkenda ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwajengea uwezo walimu wa Msingi, Sekondari na Wakufunzi wa Vyuo vya Ualimu kuhusu matumizi ya TEHAMA kama nyenzo ya kufundishia na kujifunzia, ambapo mpaka kufikia mwaka 2021 zaidi ya walimu 1,693 walipatiwa mafunzo ambapo kati yao wakufunzi na walimu wa Sekondari na Msingi wenye mahitaji maalum ni 350.
 
Prof. Mkenda amesisitiza kuwa kupitia Mradi wa Secondary Education Quality Improvement Program (SEQUIP) itawezesha kuandaa Mkakati wa TEHAMA wa elimu ya Sekondari ambao utanufaisha makundi yote ikiwa ni pamoja na walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule 1,500 za Serikali pamoja na kuandaa moduli na miongozo ya kufundishia TEHAMA kwa walimu kazini wa shule za Sekondari.
 
Naye Mkurugenzi wa Shirika la African Child, Catherine Kimambo amesema Mradi wa TEHAMA kwa Shule za Sekondari za Serikali ni muhimu kwa kuwa unajielekeza kusaidia kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu nchini.
 
Kimambo amesema kuwa mradi huo ambao ni ushirikiano wa taasisi yake, Vodacom Tanzania na Taasisi ya Teknolojia Dare es Salaam (DIT) utawafikia wanafunzi 43, 291 katika shule 50 kutoka katika mikoa 10 ukilenga kutoa mafunzo kwa walimu 100 wa TEHAMA, kugawa kompyuta 186, vishikwambi 246, kadi za simu zenye gb 50 kila mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoka Vodacom Tanzania.Aidha watatoa mafunzo ya awali ya kidijitali kupitia wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Stholizwe Mdlalose amesema wamejiunga katika mradi huo kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora na kuongeza fursa za elimu kwa wote huku akijivunia ushiriki wa Vodacom katika kusaidia maeneo mbalimbali ya sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya mtandao kwa shule, vifaa vya kufundishia na kujifunzia zikiwemo kompyuta na uwepo wa mfumo wa ujifunzaji E- Fahamu.
 
Stholizwe amesisitiza kuwa Kupitia Vodacom Foundation, zaidi ya shule 450 nchini wanapata fursa za kujifunza kupitia mtandao ambapo mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Upatikanaji wa Huduma za Mawasiliano ya Universal (UCSAF), ambapo mwaka jana walitoa kompyuta, 1,400, na mtandao wa intaneti ulionganishwa kwa shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya nchi ambayo yamekuwa hayana huduma hiyo.