Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaagiza Wakaguzi wa ndani wa Halmashauri kufanya kazi kwa ufanisi ili kuzuia mianya ya ufujaji na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo.

Mhe. Rais Samia ametoa agizo hilo  tarehe 07 Februari, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa Bunda mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa miundombinu ya kusafisha na kutibu maji utakaogharimu shilingi Bilioni 10.6 utakapokamilika, katika viwanja vya Shule ya Msingi Miembeni, wilayani Bunda Mkoani Mara.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka Wakaguzi hao kufanya ukaguzi wa hesabu za fedha za miradi ya maendeleo mapema na kwa kila hatua badala ya kusubiri ukaguzi kufanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mhe. Rais Samia pia ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara kuzuia vitendo vya rushwa kwa kufuatilia hatua zote za matumizi ya fedha katika miradi  pindi fedha za miradi zinapokuwa zimetolewa badala ya kungoja ripoti ya Mkaguzi wa Mahesabu ndipo wafuatilie.

Vile vile, Mhe. Rais Samia amekemea ucheleweshwaji wa miradi mbalimbali mkoani humo kutokana na ubinafsi na ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watendaji Serikalini.

Mhe. Rais Samia amewataka viongozi kusogeza huduma muhimu kwa wananchi na isisubiriwe hadi kufanyika kwa mgao wa maeneo ya utawala.

Aidha, Mhe.Rais Samia amewataka wale wote waliopewa nafasi za uongozi kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuwataka wananchi kuwaunga mkono na kushirikiana nao ili waweze kutoa huduma kikamilifu.

Mhe. Rais Samia amewaonya viongozi wa mkoa wa Mara kuwa iwapo Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo na fedha hizo kukaa kwa kipindi cha miezi 6 hadi mwaka bila kutumika kwa sababu za kuvutana, fedha hizo zitarudishwa Serikalini kwa matumizi mengine.

Awali akiwa njiani kuelekea Bunda, Mhe. Rais Samia amewasalimia wananchi wa eneo la Butiama na kuwaahidi wananchi hao kuwa pamoja na na miradi mbalimbali iliyotekelezwa wilayani humo Serikali itaendelea kuwaletea maendeleo zaidi.

Aidha, akiwa wilayani Butiama, Mhe. Rais Samia pia ametembelea kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mhe. Rais Samia amemaliza ziara ya siku nne mkoani Mara na kuwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa mapokezi makubwa waliyompa muda wote akiwa ziarani mkoani humo.

Jaffar Haniu
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.