Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Ally Hapi pamoja na wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kijitathmini kama wanafaa kuendelea na nyadhifa zao.

Pia, ameagiza watu waliohusika na ujenzi wa mradi wa makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Bunda vijijini kukaa pembeni kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili ikiwemo rushwa hali iliyopelekea kukwama kwa mradi huo licha ya Sh400 milioni kutolewa kwaajili ya mradi huo.

Rais Samia ametoa maagizo hayo mjini Musoma  Jumapili Februari 6, 2022 baada kupokea taarifa mbalimbali juu ya kukwama kwa miradi ya maendeleo mkoa wa Mara tatizo ambalo amesema kuwa ni sugu.

Amesema kuwa inasikitisha kuona kuwa miradi mingi ya maendeleo inashindwa kukamilika kwa wakati huku kukiwa na uongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya hali ambayo inaonyesha kuwa viongozi hao wameshindwa kutimiza wajibu wao.

"Mkuu wa mkoa ni kama uliota maana leo nilikuwa nimepanga nikufyatue hapahapa bahati yako umeeleza matatizo haya ya kukwama kwa maendeleo ina maana unafanya kazi na matatizo haya unayajua na umenoyesha umechukua hatua gani una bahati" amesema Rais Samia

Amesema kuwa matatizo ya kukwama kwa maendeleo ya mkoa wa Mara yanasababishwa na viongozi waliopo Mara ambao amedai kuwa ni wabinafsi na wabadhirifu hivyo hataweza kumvumulia kiongozi yeyote anayekwamisha maendeleo.

Mbali na kuwataka viongozi hao kujitathmini lakini amesema kuwa suala la utendaji kazi wa viongozi hao anakwenda kulifanyia kazi na maamuzi atayatoa baada ya watu wake kufanya uchunguzi.

Kuhusu wakurugenzi wa halmashauri nchini Rais Samia amesema kuwa wakurugenzi hao walipewa muda wa matazamio ambao unaisha Februari 18 mwaka huu na kwamba tayari amemuagiza Waziri wa Tamisemi kumpa taarifa ya kila mkurugenzi ili aweze kufanya uchambuzi wa nani anabaki na nani anaondoka.

Amemuagiza RC Hapi kuvunja mikataba ya makandarasi wanaojenga miradi ya barababara za Makutano Sanzte yenye urefu wa kilomita 50 kwa gharama ya zaidi ya Sh60 bilioni pamoja na wa barabara ya Musoma Makojo yenye urefu wa kilomita 5 kwa gharama ya Sh8 bilioni.

Amesema kuwa umefika muda sasa miradi ya barabara itolewe kwa makandarasi wenye uwezo kuliko ilivyo sasa ambapo miradi hiyo ya barabara mkoani Mara imechelewa kwa sababu kadhaa ikiwemo uwezo mdogo wa makandarasi ki fedha na vifaa.

Rais Samia amefikia mamauzi hayo baada ya miradi hiyo kushindwa kukamilka wakati ambayo ni barabara ya Makutano Sanzate ilitakiwa kukamilika mwaka 2015 huku barabara ya Musoma mokojo ilikuwa ikitakiwa kukamilika mwezi Julai mwaka jana.

Kuhusu ombi la Mkuu wa Mkoa wa Mara la kufumua halmashuriza mkoa huo, Raais Samia amesema kuwa suala hilo lazima lifanyiwe kazi kwani serikali haiwezi kuwang'ang'ania watu wanaokwamisha maendeleo.