Rais Samia Ashuhudia Utiaji Saini Mikataba Sita Ya Maendeleo Nchini Ufaransa
Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Zanziba
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan yuko ziarani nchini Ufaransa ambako katika ziara hiyo ametia saini mikataba sita ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini.
Hayo yameelezwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akiwa Zanzibar wakati akitoa taarifa yake ya wiki kuhusu sera, mipango na utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo mbalimbali nchini ambapo alisema kuwa Rais Samia amehudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaojadili kuhusu Raslimali Bahari Duniani ambapo akiwa nchini humo tayari amesaini miradi sita ya maendeleo ya kipaumbele.
“Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo (Agence Francaise de Development-AFD) imetoa shilingi bilioni 464.1 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka ya Gongolamboto” alisema Msigwa.
Aliongeza “Mkataba mwingine ni shilingi bilioni 208.6 kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa kifedha wa Benki ya Kilimo (TADB) ili wakulima waweze kukopeshwa na kuendesha shughuli zao za kilimo kisasa zaidi”
Vilevile, Rais Samia akiwa nchini Ufaransa amesaini msaada wa shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya kusaidia wakulima katika shughuli zao.
Aidha, Msigwa aliongeza kuwa Rais Samia na Rais wa Ufaransa walitia saini tamko la Ushirikiano wa Uchumi wa Buluu na Usalama wa Bahari na ushirikiano wa Miundombinu ya Usafiri.
Vilevile, Rais Samia akiwa nchini Ufaransa atapata fursa ya kuzungumza na Watanzania wanaoishi nchini humo sambamba na kujadili kuhusu fursa zilizopo katika nchi zote mbili.
Uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Ufaransa umedumu kwa takribani miaka 30 sasa na Tanzania imenufaika na uhusiano huo kupitia miradi ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere.
Vilevile, Msigwa aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 10 uhusiano wa nchi hizi mbili umeendelea kuwa muhimu zaidi ambapo Ufaransa kupitia AFD umeipatia Tanzania kiasi cha shilingi trillioni 1 na bilioni 538 na kusaidia katika ujenzi wa miundombinu katika sekta za nishati, elimu, kilimo, utalii na maliasili.
Aidha, Ufaransa ina miradi 40 nchini Tanzania ambayo ina thamani ya uwekezaji shilingi bilioni 167.7 na Watanzania 1,885 wamenufaika kwa kupata ajira.