Ikulu ya rais wa Ufaransa ya Élysée imetangaza kuwa, baada ya kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Russia, rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron amezungumza kwa njia ya simu pia na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky kumjulisha kuhusu mazungumzo yao.

Mazungumzo ya Macron, ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya na Putin yameonekana kutoa fursa ya mwisho ya kuuhitimisha mzozo wa Ukraine kwa njia za kidiplomasia, huku ikiripotiwa kuwa ukiukaji wa usitishaji mapigano katika eneo la Donbas mashariki ya Ukraine unaendelea kuongezeka.

Ofisi ya rais wa Ufaransa imeeleza katika taarifa kuwa, mazungumzo ya simu kati ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo na rais Vladimir Putin wa Russia yalidumu kwa muda wa saa 1:45.
Putin (kulia) na Macron

Kwa mujibu wa Ikulu ya Russia, Kremlin, katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na rais wa Ufaransa hapo jana, Putin ametaka shirika la kijeshi la NATO na Marekani "zichukulie kwa uzito" madai ya nchi yake kuhusu usalama wake, ambao ndio kiini cha mzozo wa sasa kati ya Moscow na nchi za Magharibi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Élysée, katika mazungumzo hayo ya jana Marais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Vladimir Putin wa Urusi wamekubaliana pia kufanya kila linalowezekana ili kufikiwa haraka usitishaji mapigano mashariki mwa Ukraine