Mwenyekiti Baraza la Chadema afutiwa kesi, akamatwa tena
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema (Bazecha) Hashimu Juma Issa, (63) amekamatwa na polisi muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumfutia kesi ya jinai.
Issa alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kuchapisha taarifa za uongo na kuzisambaza kwenye mtandao wa YouTube, katika kesi namba 179/2021
Alifutiwa mashtaka hayo leo Jumatano Februari 23, 2022 baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yake.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuachiwa huru, alikamatwa tena na askari Polisi waliokuwepo katika mahakama hiyo na kupelekwa Kituo cha Polisi, Oysterbay.
Uamuzi wa kumfutia mashtaka ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwanaamina Kombakono aliieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa lakini Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Mshtakiwa huyo amefutiwa mashtaka yake chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 20 , iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.