​​​​​​​Mwalimu wa Shule ya Msingi Kisokwe Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Albert Kaguli (43), amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana huku chanzo cha mauaji kikidaiwa kuwa wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi wilayani humo, akisema mwalimu huyo aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani huku Jeshi hilo likimtafuta Shukuran Maselo kwa tuhuma za mauaji hayo.

"Chanzo cha tukio hili inasadikiwa kuwa ni wivu wa mapenzi dhidi ya mtuhumiwa wa kosa hili, bado Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini watuhumiwa wengine wa mauaji hayo ya kikatili," alisema.

Alibainisha kuwa tukio hilo ni la tano kutokea mkoani humo mwaka huu na jeshi linaendelea kuwasaka wahalifu hao ili kuwachukulia hatua za kisheria.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Josephat Maganga, alilaani mauaji hayo na kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.