Na Amiri Kilagalila,Njombe
Polisi mkoani Njombe wamemkamata Ndugu Daniel Mwilango Mtuhumiwa wa mauaji ya Nickson Myamba (48) aliyekuwa katibu wa baraza la walei kanisa la Roman Katoliki kigango cha Parokia ya Makambako yaliyotokea tarehe 8 February 2022.Mwilango amekamatwa eneo la Doma wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa na vitu mbali mbali vya marehemeu ikiwemo simu ya mkononi.

“Katika hali isiyo ya kawaida simu tuliyomkuta nayo mtuhumiwa ni simu ya marehemu alikuwa bado anayo yeye,kitu kingine alichokutwa nacho marehemu ni funguo mbali mbali ikiwemo na ile chumba ambacho tukio lilitokea”alisema Kamanda Issa

Kamanda Issa amesema mtuhumiwa huyo amekiri na kuonyesha vitu mbali alivyotumia katika mauaji hayo ikiwemo Panga aliliokuwa amelitupa katika choo,chuma alichotumia kupiga marehemu,ndoo na vitambaa vilivyotumika kwa ajili ya usafi wa damu kwenye chumba yalipotendekea mauaji.

Awali akifafanua juu ya tukio hilo la mauaji lililotokea katika duka la vitabu lililopo nje katika eneo la kanisa hilo,kamanda Issa amesema mtuhumiwa alijiandaa na kutumia chuma kizito kumpiga mwenzake eneo la kisogoni.

“Alipopoteza fahamu alimuongezea tena chuma kingine pigo la pili na hili pigo la pili lilimsababishia huyu Nickson Kufariki,alichokifanya huyu Daniel alitumia panga kuutenganisha mwili,alitenganisha kiwili wili,kichwa na kifua kilikuwa sehemu yake halafu na kiuno na miguu kilikuwa sehemu yake”alisema Issa

Vile vile amebainisha kuwa polisi wanamshikilia mlinzi wa kanisa hilo aliyetambulika kwa jina la Nickson Valentine kutokana na muunganiko wa kushiriki katika tukio hilo.

“Bado upelelezi unaendelea lakini sasa hivi mtuhumiwa aliyefanya tukio eneo la kigango cha kanisa Roman Katoliki eneo la Makambako yuko Mbaloni”alisema Kamanda

Aidha kamanda Issa amesema jeshi la polisi limebaini kuwa sababu za maujai hayo ni chuki za mtuhumiwa dhidi ya marehemu.

“Hizi ni chuki binafsi ambazo alikuwa nazo mtuhimiwa dhidi ya marehemu na ukimuuliza mtuhimwa anasema marehemu ni tishio la maisha yangu kwasababu amepewa kazi zangu na anamuhisi marehemu ndiye aliyesababisha yeye akaondolewa kwenye sehemu ya duka na miradi mingine na yeye aliondolewa kwasababu ya ubadhilifu na sio vinginevyo”alisema Kamanda

Kamanda Issa amesema jeshi la polisi litaendelea kulinda makanisa na kuwaomba waumini kuendelea kwenda kanisani kusali.