Na. John Mapepele
Waziri wa utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa  Februari 15, 2022 amekutana na Balozi wa Morocco nchini Mhe. Zakaria Elgoumiri na kufanya mazungumzo ya kuendeleza sekta za michezo, utamaduni na Sanaa ambapo Balozi amesisitiza serikali yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa faida ya wananchi wa nchi hizo.

Mhe. Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania na Morocco zimekuwa na uhusiano mzuri katika sekta hizo toka muda mrefu hali ambayo imewafanya viongozi wakuu wa nchi zote kufanya ziara na kubadilishana uzoefu wa sekta hizo.

Akiwa katika kikao hicho ambacho aliambatana na Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa michezo nchini Yusufu Singo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo (BMT) Neema Msitha wamekubalina na ujumbe wa Mhe. Balozi wa kuendelea kushirikiana kwenye sekta hizo.

Ameyataja baadhi ya maeneo ya kipaombele ambayo yanakwenda kufanyiwa kazi kuwa ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo, maeneo ya tamthilia na filamu pamoja na kushirikiana kwa pamoja kuandaa matamasha ya Sanaa na Utamaduni.

Mhe. Mchengerwa amewakaribisha kushiriki katika matamasha makubwa ya kihitoria ya Serengeti litakalofanyika jijini Dodoma Machi 12,2022 na Tamasha la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa Bagamoyo.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Elgoumiri amesema Serikali ya nchi yake inafurahishwa na Sera na diplomasia ya uchumi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.

Ameuomba upande wa Tanzania kukamilisha andiko iliutiaji Saini ufanyike mara moja.

“Tupo tayari kusaini andiko la kukuza ushirikiano kwenye maeneo tuliyokubaliana wakati wowote andiko litakapokuwa tayari”. Amesisitiza Mhe Elgoumiri