Marekani imeonya kuwa Urusi inaweza kuivamia kijeshi Ukraine muda wowote. 

Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, Jake Sullivan amesema uvamizi huo unaweza ukaanza kwa shambulizi la anga. 

Tangazo la Marekani linatokana na taarifa mpya za kijasusi za kuongezeka kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mipaka ya Ukraine katika wiki moja iliyopita. 

Hata hivyo, Urusi imerudia kukanusha mipango yoyote ya kuivamia Ukraine. Licha ya kukanusha, nchi kadhaa ikiwemo Marekani, Uingereza na Japan zimewataka raia wake kuondoka Ukraine mara moja. 

Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amesema muungano huo umejiandaa kwa hali yoyote ile. Marekani inapeleka wanajeshi zaidi 3,000 nchini Poland ili kuimarisha vikosi vya NATO vilivyoko huko. 

Rais wa Marekani, Joe Biden leo anatarajiwa kuzungumza kwa njia ya simu na Rais wa Urusi, Vladmir Putin kuhusu kuongezeka kwa mzozo huo.