Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetangaza kuwepo kwa mvua za wastani hadi juu ya wastani kwa msimu wa mvua za masika ambao unatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi huu.

Mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika mikoa inayopata mvua mara mbili kwa msimu hali ambayo itasaidia wakulima kuweza kupata mavuno mazuri.

Akizungumza na waandishi wa habari  Februari 17, 2021 Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Dk Agnes Kijazi amesema kuwa ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Machi katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Aprili kwa Nyanda za Kuu Kaskazini Mashariki.

Amesema mvua hizo zitakuwa na faida kwa wakulima kwani zitasabaisha unyevuvyevu wa udondo na maji yatakayovunwa kwaajili ya umwagiliaji ambao utatosheleza mahitaji ya kilimo kwa msimu husika.

Dk Kijazi ameongeza kuwa wakulima wanatakiwa kuandaa mashamba yao na kupanda mapema kwa kutumia teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani pamoja na mmomonyoko wa udongo ambao utasababisha kupoteza rutuba.

Kwa upande wa sekta ya mifugo na uvuvi, Dk Kijazi amesema kutakuwa na ongezeko la maji katika maziwa, mito na mabwawa hali hiyo itasaidia uwepo wa uzalishaji samaki vizuri, hivyo wavuvi kushauriwa kuhakikisha wanafuata ushauri wa wataalamu na miongozo ya uvuvi bora.

Pia wafugaji wameshauri kuangalia uwezekano wa kulisha mifugo yao kwa mzunguko ili kuweza kuhifadhi malisho mpaka msimu mwingine, utaratibu ambao utawasaidia kuepukana na kutafuta malisho kwa baadaye.