Dodoma, Tanzania.
Serikali imewahakikishia wakulima wa shayiri  kupata soko la uhakika kwa kuiuzia moja kwa moja  Kampuni ya Bia Tanazania TBL .

Akizungumza  baada ya kikao chake na viongozi wa TBL kilichohudhuriwa na  Naibu Waziri wa Kilimo Mhe  Anthony Mavunde, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema wamekutana na viongizi wa TBL kufuatia kauli aliyoitoa hivi karibuni jijini Arusha kuhusu TBL kiingia mikataba ya kununua shayiri moja kwa moja kutoka kwa wakulima

Mhe. Bashe amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 TBL imedhamiria kufanya uwekezaji mkubwa nchini na iliiomba serikali mambo kadhaa ambayo yangeirahishia kampuni hiyo kuwekeza.

Waziri Bashe ameyataja maombi hayo ikiwa ni pamoja na nafuu ya kodi kwa zao la shayiri kama malighafi na kupata ardhi mkoani Dodoma.

Aidha Mhe. Bashe amebainisha kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Wizara ya Fedha serikali imeikubalia TBL maombi waliyoomba.

Pamoja na kukubaliwa kwa maombi waliyoomba, TBL imekubaliana na serikali kuingia mikataba na wakulima ya kununua tani za shayiri zisizopungua 5,000 hadi 6,000 kwa mwaka kutoka kwa wakulima.

Katika utekelezaji wa makubaliano hayo tayari TBL imeingia mikataba ya ununuzi wa tani 3,000 moja kwa moja kutoka kwa wakulima.

Ili kukamilisha malengo kwa mujibu wa makubaliano serikali imeielekeza TBL kwenda wilaya ya Hanang mkoani Manyara na kuingia mikataba ya tani 2,000 na
wakulima wa huko ili kukamilisha kiwango cha chini cha ununuzi walichokubaliana na serikali ambacho ni tani 5,000.

Mbali na makubaliano hayo, Mhe. Bashe amesema serikali imekubaliana na TBL kwenye kilimo cha mkataba cha zao la zabibu.

Waziri Bashe amefafanua kuwa baada ya majadiliano TBL wamekubaliana na serikali kuingia mikataba na wakulima wa zabibu wa mkoani Dodoma na kuwaelekeza viongozi wa TBL kushirikiana na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde kukamilisha mchakato huo.

Waziri Bashe amebainisha kuwa Wizara ya Kilimo inaamini kuwa wakulima wakiwa na makubaliano ya moja kwa moja na wakulima itawasaidia wakulima wa Tanzania na TBL itarahisha kazi katika kumfikia mkulima kwani kwa sasa ili TBL imfikie mkulima.

Kuhusu hitaji la kupata ardhi, Mhe. Bashe amesema tayari serikali imeshawapa hekari 250 mkoani Dodoma.

Akitoa shukrani kwa Wizara ya Kilimo Mkurugenzi Mkaazi wa TBL Jose  Moran
amesema watafuata makubaliano waliyokubaliana na serikali kwani wamejidhatiti kuunga mkono juhudi za wakulima wa Tanzania na wataendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo.