Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Diana Edward Bundala ( Mfalme Zumaridi) kwa kosa la usafirishaji haramu wa Binadamu na Unyonyaji.

Ndugu waandishi wa Habari, tarehe 26.02.2022 majira ya 12:30hrs huko eneo la mtaa wa Buguku, kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lilimkamata Dianna Edward Bundala @ Zumaridi, miaka 39, Mkazi wa Mtaa wa Buguku-Buhongwa kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu wapatao 149.

Watu hao wametolewa na kusafirisha toka sehemu mbalimbali kisha kuwafungia nyumbani kwake ambapo alikuwa akiwatumikisha, kati yao wanaume 57, wanawake 92 na mingoni mwao wapo watoto 24, wanaokadiriwa kuwa na miaka kati ya 4-17, ambao wamekatizwa masomo kinyume na sheria, hata hivyo amekuwa akiwaaminisha kuwa yeye ni Mungu anayeponya, kufufua wafu na kutatua matatizo yao.

Awali tarehe 23.02.2022 polisi walipokea amri ya Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni iliyotaka kumkamata mzazi wa kike wa mtoto Samir Ally Abbas ayetakiwa kufikishwa mbele ya mahakama hiyo baada ya kesi ya msingi kusikilizwa. Katika utekelezaji wa amri hiyo Polisi walifika Nyumbani kwa Mtuhumiwa Dianna Edward Bundala ambapo ilidaiwa yupo mzazi wa kike wa mtoto huyo na mtoto aliyetakiwa kufikishwa mahakamni.

Aidha baada ya askari kufika eneo la tukio mtuhumiwa akiongoza wafuasi wake waliwashambulia askari na kuwazuia kufanya kazi yao, ndipo askari waliondoka eneo hilo kwa nia yakuepusha kutumia nguvu ambayo ingeweza kuleta madhara. Tarehe 26.02.2022 Askari Polisi walirudi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na kufanikisha ukamataji kwa mujibu wa sheria,

Upelelezi wa kina unaendelea ili kubaini kiini cha watu hao kukusanyika katika nyumba ya mtuhumiwa ambayo sio nyumba ya ibada wala sehemu rasmi ya kongamano. Baada ya upelelezi kukamilishwa Mtuhumiwa pamoja na washirika wake katika kutenda kosa watafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Ndugu waandishi wa habari; - Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea kutekeleza maelekezo ya Mwendesha Mashitaka Taifa (DPP) ya kuwaachia jumla ya watuhumiwa 36 wa makosa ya vitendo vya kujihusiha na Ugaidi ambao wamekidhi masharti ya dhamana. Pia tutawaachia watakaokidhi Vigezo vya dhamana.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa baadhi ya watu kuacha kutumia mwanvuri wa dini kuwaadaa wananchi wawapo na matatizo ya kijamii hususani magonjwa na hali ngumu ya maisha. Pia Jeshi la Polisi linawashukuru wananchi ambao waliona viashiria vya kinyonyaji na kutoa taarifa Polisi.


IMETOLEWA NA;-

Ramadhan Ng’anzi – SACP

KAMANDA WA POLISI (M) MWANZA