Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imesema Ijumaa Februari 18, 2022 itatoa uamuzi iwapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wana kesi ya kujibu au la katika kesi ya ugaidi inayowakabili.

Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo amesema hayo jana  Jumanne Februari 15, 2022 baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahaka kuwa wamefunga kesi hiyo kwa shahidi wa 13 kuhitimisha ushahidi wake.

Shahidi huyo wa 13 wa upande wa mashtaka ambaye ni Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila alimaliza kutoa ushahidi baada ya kuhojiwa maswali ya dodoso na upande wa utetezi.

Baada ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, Wakili wa Serikali Robert Kidando aliiambia Mahakama kuwa wamefunga ushahidi na kuiomba ione kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.

“Baada ya ushahidi wa shahidi huyu wa kumi na tatu tunaialika Mahakama yako chini ya kifungu 41 (1) cha sheria ya Uhujumu Uchumi ione washtakiwa wote wanne wana kesi ya kujibu hivyo hatua nyingine kwaajili ya kujitetea ifuate kwa upande wetu tunafunga kesi hii” alisema Wakili Kidando

Hata hivyo, baada ya upande wa mashtaka kutoa ombe hilo, upande wa utetezi kupitia Wakili Peter Kibatala uliomba kupewa nafasi ya kufanya mawasiliano ya mdomo pamoja na kupewa mwenendo wa kesi.