Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema hakuna mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kata za Inyala, Itewe, Ilungu na Hifadhi ya Kitulo iliyoko mkoani Njombe.

Ameyasema hayo jana bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Mhe. Oran Manase Njeza aliyeuliza lini Serikali itamaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TFS/TANAPA na wananchi wa Kata za Inyala, Itewe na Ilungu.

Amefafanua kuwa changamoto iliyopo katika hifadhi hiyo ni kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi kwa wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuchumi na si mgogoro wa ardhi kama inavyosemwa.

Ameongeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa ardhi wananchi wamekuwa wakidai maeneo waliyokuwa wanatumia kabla ya Hifadhi ya Taifa Kitulo kuanzishwa mwaka 2005 yarudishwe kwao ili kukidhi mahitaji zaidi ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.