Waziri Mkenda Anena Mambo Mazito Akimkabidhi Ofisi Waziri Mpya Wa Kilimo
Na Mathias Canal, Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amekabidhi Ofisi kwa Waziri mpya wa Kilimo Hussein Bashe huku alieleza kuwa amekabidhi kwa mtu anayejua vizuri.
Hayo ameyasema jijini Dodoma tarehe 11 Januari 2022 wakati akikabidhi Ofisi kwa Waziri huyo Mara baada ya kuapishwa rasmi jana ambapo ametumia nafasi hiyo kuwashukuru watumishi wa wizara hiyo kwa ushirikiano waliompa na kuwaaga.
“Nakabidhi ofisi kwa mtu anayejua wizara hii maana nilipokuja hapa nilimkuta mheshimiwa Hussein Bashe tumefanya kazi pamoja anaifahamu vizuri ofisi na mengi yaliyomo humu anayafahamu, nakutakia kila la heri kwenye utumishi wako,”.amesema Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda wakati akikabidhi ofisi.
“Mimi na Bashe tumefanya kazi pamoja kwa ushirikiano mkubwa Kuna wakati mambo yalikuwa yakiwaka moto tunakutana haraka usiku ili kujadili na kutoka na msimamo mmoja,” amesema Profesa Mkenda
Amesema kilimo ni changamoto kubwa lakini kwa sasa kipo mikono salama na kuwataka waliobaki kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuondoa baadhi ya changamoto zilizobaki.
Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru watumishi wa wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliompa wakati wa mchakamchaka wa utekelezaji majukumu yake.
Akizungumza Mara baada ya kukabidhiwa ofisi, Waziri Bashe amesema katika kipindi cha mwaka mmoja walichofanya kazi kwa pamoja misingi mizuri imejengwa ambayo yeye ataendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kilimo kinasonga mbele.
“Tumefanya kazi mwaka mmoja ambao tumejenga misingi mizuri ambayo tutaendelea nayo sababu najua juhudi tulizofanya kufikia sehemu nzuri, tuna changamoto nyingi zinatukabili hivyo lazima tuzifanyie kazi, kwa kipindi cha mwaka mmoja nimepata ujuzi mkubwa kutoka kwako hivyo nakuahidi hakuna kilimo bila teknolojia wala Sayansi hivyo nitaendelea kukusumbua” Amekaririwa Mhe Bashe
Kadhalika, Waziri Bashe amemuimba Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Adolf Mkenda kutenge fedha kwa ajili ya kwenda kusomesha wataalamu wazuri wa kilimo nje ya nchi.