Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya Majanga na Maafa nchini kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa cha kisasa (Tanzania Centre of Excellence in Disaster Management).  

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea na kukagua Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharula kilichopo katika ofisi hiyo  Desemba 31, 2021 Jijini Dodoma kwa lengo la kupokea taarifa na hatua zinazochukuliwa katika kuboresha utendaji wa kituo hicho.

Waziri Mhagama alieleza kuwa kati ya mambo mazuri yaliyofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa katika mwaka wa 2021 ni pamoja na ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa cha kisasa kinachojengwa eneo la Nzuguni ‘B’ Jijini Dodoma.

“Ofisi ya Waziri Mkuu tunajivunia na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za ujenzi wa mradi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa ambacho kitasaidia kuimarisha uwezo wa usimamizi wa maafa katika sekta zote hapa nchini kwa ajili ya maendeleo endelevu,” alisema Waziri Mhagama

“Ujenzi wa kituo hicho ni dhamira ya serikali katika kuhakikisha inazingatia namna njema ya hatua za kuchukua tahadhari dhidi ya majanga na maafa yanapojitokeza,” alisema

Aliongeza kuwa, Katika kutekeleza mpango huo Serikali imeendelea na azma ya ujenzi wa Kituo cha Tiafa cha Usimamizi wa Maafa nchini kwa kuingiza tena mpango wa ujenzi wa kituo hicho katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020 – 2025) katika Ibara ya 107 kipengele (h) ikiwa na lengo la kuhakikisha vyombo vinavyoshughulika na maafa vinakuwa na mpango wa utayari wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Sambamba na hayo Waziri Mhagama alieleza kuwa kituo hicho kitasaidia kuimarisha mfumo wa usimamizi wa maafa na kuwezesha uwepo wa vifaa na zana za kisasa katika utoaji wa huduma za usimamizi wa maafa nchini, kuwa na mfumo wa kisayansi wa kufuatilia mwenendo wa majanga na kutoa maelekezo ya hatua za kuchukua kwa wakati kwa ajili ya tahadhari za awali, kuimarisha mfumo wa kitaasisi wa kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya maafa, kuwa na rasilimali za kutosha na kuimarisha ushirikiano na wadau katika utekelezaji wa dhana nzima ya mzingo wa maafa kwa ajili ya kuwa na jamii yenye uchumi stahimilivu pamoja na kituo hicho cha usimamizi wa maafa kuwa cha mfano kwa ajili ya jamii yenye ustahimilivu na uchumi endelevu nchini.

Baada ya ziara hiyo ya kutembelea na kukagua Kituo hicho cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharula, Waziri Mhagama amewataka wadau kutoka katika sekta mbalimbali wanashughulikia masuala ya majanga na maafa kuwa na mfumo wa Kanzi Data (Data Base) ili kujua namna walivyorejesha hali katika maeneo yaliyokubwa na majanga na maafa.