Na WMNN, Dar es Salaam

KUTOKANA na mauaji ya kijamii yanayoendelea nchini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amepanga kukutana na Watendaji Wakuu wa Jeshi la Polisi ili kujadili jinsi ya kudhibiti mauaji hayo.

Waziri Masauni amesema katika kikao hicho pia kitajadili jinsi ya kulifanya Jeshi la Polisi kuwa la kisasa katika kudhibiti matukio mbalimbali kiuhalifu nchini. 

Akizungumza katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi (Forensic Bureua), jijini Dar es Salaam, leo, Masauni amesema lengo kuu la kukutana na viongozi hao siku ya Jumatatu Januari 31, 2022, ni kupata taarifa ya uchunguzi wa mauaji ambayo waliushaanza na kujua jinsi gani matukio hayo yanaweza kumalizwa katika jamii.

“Siku ya Jumatatu nitakua na kikao na Viongozi wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na IGP pale Wizarani kwa ajili ya kupitia matokeo ya kazi ya uchunguzi ambayo wanaifanya na Serikali tunategemea waifanye ili tuweze kuwajulisha wananchi juu ya hayo matukio yote ili tujue tulipofikia, hatua zake ni zipi, na mafanikio yake ni yapi na mikakati kuweza kuhakikisha mambo kama haya ya mauaji tunaweza tukayapunguza katika siku za usoni,” alisema Masauni.

Waziri Masauni aliongeza kuwa, lengo kuu la ziara yake ni kutaka kuona Kamisheni hiyo ya Uchunguzi jinsi inavyochunguza na kudhibiti mauaji pamoja na kuhakikisha wahalifu wanapatikana kwa haraka na kwa ufanisi zaidi. 

Aidha, Masauni alizungumzia kuhusu uhalifu wa kimtandao ambapo aliliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka wanaosajilia watu laini za simu, wanaochafua viongozi na wanaosambaza picha chafu mitandaoni.

Alisema suala la uhalifu wa kimtandao limekuwa kubwa katika siku hizi za karibuni na kadiri siku zinavyokwenda mbele na teknolojia inavyozidi kutanuka ndipo matatizo ya uhalifu wa kimtandao yanavyoongezeka, hivyo ni lazima Jeshi liwe tayari kukabiliana na mabadiliko ya aina yoyote katika kudhibiti uhalifu huo ambao haukubaliki na hauwezi kuachwa uendelee.

“Wapo watu wamekuwa wakitumia mitandao vibaya kudhalilisha watu wengine, wengine ni watu wazima wanaweza kuwa hata wazazi wao, wapo wanaotumia mitandao kufanya wizi na uitapeli kwa raia wengine, wapo watu ambao wanajadili mambo ambayo yapo kinyume na maadili, desturi za watanzania, ambapo haya yote yanayoendelea kufanyika lazima yadhibitiwe na Jeshi la Polisi, kwahiyo kuna haya ya kuhakikisha haya yote yanafanyika kwa kasi zaidi,” alisema Masauni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhalifu wa Kimtandao, SSP Joshua Mwangasa, alimshukuru Waziri huyo kwa kutembelea Kamisheni hiyo na kuahidi kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa.

“namuahidi Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla hili suala tutalifanyia kazi usiku na mchana, amejionea mwenyewe jinsi tunavyofanya kazi na jinsi gani tunavyopambana na uhalifu wa kimtandao, kwahiyo cha msingi ni kupokea maelekezo na kuyafanyia kazi ili changamoto nyingi sana tuweze kuzifanyia kazi na  kuzimaliza,” alisema SSP Mwangasa.

Waziri Masauni alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoimarisha vyombo vya ulinzi na usalama nchini vikiwemo vyombo vilivyopo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi vimeweza kujengewa mazingira mazuri katika kipindi cha uongozi wake kwenye eneo la stahiki na maslahi ya askari wetu kwenye eneo la kupandishwa vyeo, kupunguza changamoto ya ajira kwa kuajiri vijana wapya na kuwapa vifaa vya kisasa vinavyoweza kuweza kufanya kazi ambazo ameziona katika ziara yake katika Kamisheni hiyo.