Na Janeth Mesomapya
Waziri wa Nishati, Mh. January Yusuph Makamba ametoa wito kwa serikali ya India na wawekezaji wa nchini humo kutembelea nchini Tanzania ili kutazama fursa zinazopatikana kwenye maeneo mbalimbali ya sekta ya nishati ikiwa ni pamoja na zile za kitalu cha Mnazi Bay North ili kufanya uwekezaji.

Waziri Makamba ameyasema hayo, Jumatano, Januari 5, 2022 alipokutana na Balozi wa India nchini Tanzania Mh. Binaya S. Pradhan katika ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam. Mazungumzo yao yalilenga kujadili ushirikiano kwa kisekta baina ya Tanzania na India.

Alieleza kuwa zipo fursa za uwekezaji kwenye kitalu hicho ambazo zinahitaji uwekezaji wa haraka na hivyo wafanyabiashara na wawekezaji hao wajitokeze ili kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) katika kuzitumia fursa husika.

Vivyohivyo, alisema zipo fursa za uwekezaji kwenye miradi ya nishati ya jua na ujenzi wa maghala ya kutunzia mafuta ambayo ni hitaji kubwa kwa Tanzania na inaweza kutumika kimkakati kusambaza mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Nawakaribisha sana wawekezaji wa India kuwekeza katika fursa za maghala ya mafuta kwa kushirikiana na kampuni ya kuhifadhi mafuta (Tiper) kwa kutumia miundombinu yake ambayo tayari imeshajengwa, kikubwa ikiwa ni kuzingatia uboreshaji wa miundombinu hiyo,” amefafanua Waziri Makamba.

Kwa upande wake, Balozi Pradhan alisema Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wake kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana nchini.

Alieleza kuwa kwa sasa Serikali hiyo inatazamia kuwekeza nchini Tanzania kwenye eneo la maghala ya mazao ya petroli, fursa zinazotokana na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Chongoleani Tanzania (EACOP) pamoja na miradi ya umeme wa jua (solar) ukiwemo ule wa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

“Serikali ya India kwa kushirikiana na sekta binafsi imejipanga kuendelea kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali ya kimaendeleo duniani kote, ikiwemo nchini Tanzania,” aliongeza.