Na. Angela Msimbira Njombe
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais –TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kumrudisha makao makuu na kumpangia kazi nyingine aliyekuwa Meneja wa TARURA Mkoa wa Njombe Mhandisi Ibrahim Kibasa aliyehamishiwa Mkoa wa Ruvuma.
Ametoa maelekezo hayo leo wakati akikagua ujenzi wa Daraja la Ruhiji lenye urefu wa mita 22 na upana wa mita 8 lililopo katika barabara ya mabatini – Ramadhani yenye urefu wa kilometa 1.4 linalounganisha kata ya Njombe Mji na Kata ya Ramadhani, Halmashauri ya Njombe Mji, Mkoani Njombe.
Waziri Bashungwa amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Daraja hilo ambalo lilianza kujengwa Mei 21, 2020 na lilitakiwa kukamilika Septemba, 2020
“ Kuna uzembe mkubwa katika ujenzi wa daraja hili ambalo ni kiungo muhimu kwa wananchi wa maeneo haya kwa kuwa wanatumia daraja hili kwa ajili ya kusafirisha mazao yao sokoni, hivyo kususua kwa ujenzi daraja hatuwatendei haki wanachi” amesema Bashungwa
Waziri Bashungwa amemuagiza Meneja TARURA Mkoa wa Njombe Mhandisi Gerald Matindi kuhakikisha anamsimamia mkadarasi anayejenga daraja hilo kukamilisha kwa muda uliopangwa , pia amempa muda wa miezi sita kutatua changamoto za miundombinu katika Mkoa Njombe
Akiwa katika kijiji cha mbalache, kata mbalache , Halmashauri ya Wilaya ya Makete waziri bashungwa ameagiza kuanza mara moja kwa ujenzi wa barabara ya lupila – Kipengere yenye urefu kilometa 5 kwa kiwango cha changarawe na kutoa wiki mbili mkandarasi kuanza ujenzi huo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongezea TARURA bajeti kutoka shilingi bilioni 8.44 mwaka 2022/2021 hadi milioni 22.529 mwaka 2021/2022