Ripoti kutoka Afrika Kusini zinasema kuwa kikosi cha zimamoto kimefanikiwa kudhibiti kwa kiasi fulani moto mkubwa uliokuwa ukiunguza jengo la Bunge la nchi hiyo jijini Cape Town.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, moto huo ulianza lalfajiri ya leo Jumapili Januari 2, 2022.

Kikosi cha zimamoto kilikuwa bado kinaendelea kupambana na moto huo ambao chanzo chake bado hakijajulikana.

Hadi asubuhi ya leo, moshi ulikuwa bado ukifuka kutoka kwenye moja ya majengo kadhaa ya Bunge katika mji wa Cape Town.

Waziri wa Kazi za Umma na Miundombinu Patricia De Lille amewaambia waandishi wa habari kwamba hakuna ripoti za majeraha yoyote.

Vilevile Jean-Pierre Smith, mjumbe wa kamati ya Meya wa Cape Town inayohusika na ulinzi na usalama, amewaambia waandishi wa habari kuwa wazima moto wamegundua nyufa kwenye ukuta na paa moja lililoporomoka
.