WATU watano wa kijiji cha Kibuye, Kibondo mkoani Kigoma wamefariki dunia baada ya kujeruhiwa na radi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha ikiambatana na radi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, James Manyama, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 12:00 jioni na kusababisha vifo vya watoto wanne wanaokadiriwa kuwa na miaka mitano na 10 na mwanamke mwenye miaka 50.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Baseka Japhet (10) mwanafunzi wa darasa la tano, Goma Jeremia (5), Rock Ramadhani (5), Alam Paschal (9) na Anatoria Muhoza (50), mkulima mkazi wa kijiji cha Kibuye.
Kamanda alisema watoto hao walikuwa nyumbani wanacheza chini ya mti wa mwembe wakati mvua inaendelea kunyesha ndipo walipopigwa na radi na kusababisha vifo vyao, huku Muhoza akipigwa na radi akiwa shambani akiendelea na shughuli za kilimo.
Alisema miili ya marehemu wote imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Manyama alitoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Kigoma hasa katika kipindi hiki cha mvua, kujikinga ndani ya nyumba zao na waepuke kujikinga mvua chini ya miti.