Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema katika hotuba yake aliyoitoa hivi karibuni hapakuwa na jambo la kukashifu wala kudharau juhudi za Serikali bali alikuwa anasisitiza ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Januari 3, 2022 jijini Dodoma, Ndugai amesema “Katika mazungumzo yale baadaye ikatengenezwa clip na baadhi ya watu wakakatakata mambo, wakawasilisha ujumbe nusu, ujumbe nusu ule umesababisha mjadala mkubwa katika nchi yetu, ambao mjadala umesababisha usumbufu wa hapa na pale” amesema Ndugai nakuongeza
“Kwenye ujumbe wangu, hakukuwa na lolote la kudharau juhudi za serikali, serikali ni baba yetu na mama yetu, tunahitaji serikali na tunaiunga mkono na niliwataka wenzangu kujiimarisha kiuchumi, tulipe kodi na tozo, huo ndiyo ulikuwa msisitizo wa hotuba yangu.
"....Na huu ndio ulikuwa msisitizo wa hotuba yangu ili tuisaidie Serikali yetu na nchi kujitegemea zaidi. Na nikasema kwa nini sisi Bunge tulipitisha Tozo.
“Nikasema, endapo wenzetu mnaona wabunge tulifanya jambo baya kupitisha tozo, basi mtatuhukumu huko mbele. Sikumaanisha taasisi nyingine yoyote. Kufuatia hilo likajitokeza jambo la kama vile Spika anapinga mkopo wa Serikali wa tril 1.3, hilo binafsi limeniuma sana,” Spika Job Ndugai.