KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amemtaja Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa turufu ya maendeleo ya Watanzania kutokana na falsafa iliyobeba mambo matatu anayoyatumia katika uongozi wake.

Mambao hayo ni upangaji, usimamiaji na utekelezaji.

Shaka aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akipokea tuzo ya kumpongeza Rais Samia kwa utendaji mzuri, iliyotolewa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema Rais Samia amekuwa turufu ya maendeleo ya watanzania kutokana na falsafa tatu anazozitumia katika uongozi wake ambazo ni upangaji, utekelezaji na usimamiaji.

Kwa mujibu wa Shaka, hayo yamejidhihirisha katika uongozi wake kwa kipindi cha miezi tisa ambapo mambo makubwa yamefanyika.

Alieleza katika kipindi hicho umeshuhudiwa utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025, kwamba wanaamini kufikia mwaka 2025 utekelezaji utazidi asilimia 100.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Tawi la UDSM, Isack Sambuli, alisema uamuzi wao huo unatokana na kuguswa na mambo makubwa anayoyafanya Rais Samia ambayo moja kwa moja yanawagusa wanafunzi wa elimu ya Juu na Watanzania kwa ujumla.

Alisema miongoni mwa mambo hayo makubwa ni pamoja na kuongeza fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya Juu.

Sambuli alisema uamuzi wao huo haukulenga kutaka kutazamwa kwa ajili ya uteuzi wa uongozi Bali wamelenga kutazama uhalisia wa mambo makubwa.