Na Lucas Raphael,TABORA
SERIKALI imeanza kutekeleza miradi 18 ya maji yenye thamani ya sh bil 5.2 katika vijiji 44 vilivyoko katika wilaya 7 za Mkoa wa Tabora kwa lengo la kumtua mama ndo kichwani.

Mikataba 10 ya utekelezaji miradi hiyo imesainiwa juzi mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi ambapo jumla ya Wakandarasi 7 wamepewa jukumu la kutekeleza miradi hiyo.

Dkt balozi Batilda aliwataka Wakandarasi hao kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kwa ubora unaotakiwa huku akisisitiza kumaliza miradi hiyo kwa wakati ili kutimiza lengo la Mheshimiwa Rais Samia la kumtua mama ndoo kichwani.

Alibainisha kuwa miradi 13 kati ya 18 inatekelezwa na serikali kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 na iliyobaki inatakelezwa kwa fedha za PforR.

‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea fedha za UVIKO 19 kiasi cha sh bil 2.95 na sh bil 2.29 za P4R kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji 44 vilivyoko katika wilaya zote za Mkoa huu’, alisema.

Aliagiza Mameneja wa RUWASA wa wilaya zote ambako miradi inatekelezwa kufuatilia na kusimamia kwa karibu zaidi miradi hiyo ili utekelezaji wake ufanyike kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza mikataba yao.

Naye Meneja wa RUWASA Mkoani hapa Mhandisi Hatari Kapufi alisema kuwa miradi hiyo iliyoko chini ya wakala huo ni muhimu sana kwani itasaidia kuunguza kwa kiasi kikubwa kero ya maji miongoni mwa jamii katika wilaya hizo zote.

Alitaja Wakandarasi walioingia nao mkataba kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo kuwa ni Nassa Driling & General Supplies, Elegance Developers Co.Ltd, Monmar and Sons Co.Ltd, Jisham & Construction Co.Ltd, Kalago Enterprises Co.Ltd, Build Tech Engineering na Water Solutions Drilling Co.Ltd.

Afisa wa TAKUKURU wa Mkoa huo anayesimamia Kitengo cha Uchunguzi, Edna Adrian,alitoa onyo kwa mtu yeyote atakayetumia vibaya fedha za miradi hiyo huku akisisitiza kuwa watapita kukagua kila hatua ya utekelezaji miradi hiyo.

Naye Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani hapa Majaliwa Bilal alisema kuwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya CCM, hivyo akawataka wakandarasi kuzingatia maelekezo ya mikataba yao ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati na wananchi waanze kuyatumia.

Akiongea kwa niaba ya Wakandarasi wenzake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Monmar and Sons ya Mkoani Tabora Steven Fikiri alishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapa kazi hiyo ili kuwaletea maji wananchi.

Aliahidi kuwa watatekeleza kazi hiyo kwa weledi na ubora uliokusudiwa ili azma ya serikali ya kumaliza kero ya maji kwa jamii iweze kutimia.