Raia nchini Sudan wamefunga maduka na kuziba barabara katika mji mkuu Khartoum kuendeleza kampeni ya uasi wa kiraia dhidi ya utawala wa kijeshi.
Hatua hiyo imejiri siku moja tu baada ya vikosi vya usalama kufyatua risasi na kuwaua waandamanaji saba, ikiwa ni mojawapo ya machafuko mabaya tangu mapinduzi ya Oktoba 25 ambayo yalichelewesha mchakato wa mpito wa kidemokrasia.
Kulingana na takwimu za madaktari, idadi ya waliouawa jana inafikisha jumla ya waandamanaji ambao wameuawa hadi 71 kufikia sasa.
Wanaharakati wanaoyaongoza maandamano hayo Sudan na kupigania demokrasia wametoa wito wa kufanyika maandamano ya siku mbili kuanzia leo.
Baada ya mauaji ya jana, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Volker Perthes ameshutumu matumizi ya risasi za moto.
Vilevile ubalozi wa Marekani mjini Khartoum umelaani kile ulichokitaja kuwa mbinu za machafuko za vikosi vya Sudan dhidi ya waandamanaji.