Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kusimamia miradi ya miundombinu kikamilifu kwa kwa kuweka mikakati maalum ya kuitembelea na kufanya vikao vya mara kwa mara ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati na viwango.

Akizungumza Mkoani Kigoma  baada ya kukagua mradi wa upanuzi wa bandari za Kibirizi na Ujiji Prof. Mbarawa ametoa rai kwa TPA kupitia upya miradi ya wanayotekeleza nchini kote na kwa kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuongeza idadi ya wahandisi kweye miradi hiyo.

“Mamlaka ina miradi nchi nzima lakini miradi niliyotembelea leo ya bandari za ziwa Tanganyika imekuwa ikisuasua sana, mhandisi mshauri anaandika barua ya vikao TPA hamuonekani, kwa namna hii hatutafika na sio sawa’ Amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amebainisha kuwa kukamilisha kwa miradi hiyo kutarahisisha shughuli za usafirishaji baina ya Kigoma na nchi Jirani zinazozunguka Mkoa huo ikiwemo Jamhuri ya Kidekrasia ya Kongo (DRC) na Burundi kwani kupitia bandari hizi usafirishaji utarahisishwa.

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua maendeleo ya ukarabati ya Meli ya MT Sangara na kuitaka Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kusimamia mradi huo kwa kukagua kila hatua ya ukarabati huo ili kupata thamani ya fedha na kuepuka kufungiwa vipuri visivyokidhi vigezo kulingana na mkataba.

Naye Meneja wa Bandari ya Kigoma, Manga Gasaya amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa tathmini itafanyika na Mamlaka itatoa taarifa ya mikakati iliyojiwekea kukamilisha miradi hiyo ikiwemo ratiba za ukaguzi.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Allen Butembelo amesema ukarabati wa meli ya MT. Sangara umefikia asilimia 40 na kuahidi kuendelea kuusimamia ili ukamliike kwa wakati.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa yuko Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki kikao kitakachowakutanisha Mawaziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Fedha wa Tanzania na Burundi kujadili miradi ya maendeleo hususani Reli ya Uvinza-Musongati-Gitega.