Na WMJWM, Dodoma

Vitendo vya ukatili ikiwemo mauaji vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali nchini vimeisukuma Serikali kuwaangukia viongozi wa dini kushirkiana kukemea vitendo hivyo katika nyumba za ibada.

Akiongea na waumini wa Kanisa la Afrikan Inland Church Tanzania (AICT) Kizota Jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, amesema sasa wa nyumba za ibada kuhubiri na kukemea Vitendo vya kikatili ili kuinusuru jamii na madhila ya watu kutoana uhai kiholela.

Amesema pamoja na Serikali kutekeleza mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto ni wakati sasa wa jamii na wadau wote ikiwemo viongozi wa dini zote kushirikiana kutokomeza vitendo vya ukatili kwani serikali peke yake haiwezi kufanikiwa endapo makundi mengine katika jamii yataachwa nyuma.

“Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya ya kutisha kwa watu kutoana uhai kwa sababu ambazo unajiuliza na kushindwa kupata majibu kwa haraka, Serikali ina imani wanaofanya vitendo hivyo wako kwenye jamii na wote wana dini zao, rai yetu tunaomba Viongozi wa Dini tulibebe hili kwa pamoja” Amesema Dkt. Gwajima.

Aidha, ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambayo ina dhamana la kushughulikia maslahi mapana ya jamii ikiwemo kukemea vitendo vyote vya uvunjifu wa haki na ustawi wa binadamu.

Katika mahubiri yake Mchungaji wa kanisa hilo Mch. John Sweya amesema mauaji hayo ni kinyume cha haki za binadamu na maelekezo ya vitabu vitakatifu ambapo anayeweza kutoa uhai wa binadamu ni Mungu pekee.

Amesema vitendo hivyo vinasababishwa na wanajamii kukiuka maelekezo ya Mwenyezi Mungu yanayosisitiza upendo miongoni mwao.

Ameahidi kupitia kanisa hilo kushirikiana na Serikali kupitisha elimu kwa Umma kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili yakiwemo mauaji.

“Waumini tumrudie Mungu na kumuomba ili kutengeneza Taifa lenye upendo” amesema Mchungaji Sweya.

Kwa siku za hivi karibuni kumeibuka wimbi la baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali ya nchi kuuana na kusababisha taharuki.

Serikali iliandaa na kutekeleza Mpango wa Tiafa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto MTAKUWWA wa mwaka 2017/18 hadi 2021/22 unaolenga kutokomeza vitendo vya ukatili kwa angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.