Na Mwandishi Maalumu
TAASISI, Wakala na Mashirika ya Umma nchini yamesisitizwa kuutumia vizuri Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Msajili wa Hazina (OTRMIS), kwa kuwa utasaidia kurahisisha uchambuzi wa taarifa za kifedha za Taasisi, Wakala na Mashirika ya umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Aidha, imeelezwa kwa kiasi kikubwa matumizi ya mfumo huo wa kielektroniki utapunguza matumizi ya shajara na hivyo fedha hizo kutumika kwa matumizi mengine ya taasisi hizo.
Hayo yamesemwa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi cha kuingiza taarifa za hesabu za robo mwaka katika Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Msajili wa Hazina, kinachofanyika jana jijini Dar es Salaam kikishirikisha wahasibu, maafisa mipango na maafisa Tehama kutoka taasisi na mashirika yote 237 yaliyopo chini ya Msajili wa Hazina.
Msajili wa Hazina pia amesema OTRMIS itasaidia taarifa za kifedha kwenye taasisi na mashirika ya umma kuwasilishwa na kufika kwa haraka na kwa wakati katika Ofisi ya Msajili wa Hazina yenye jukumu la kusimamia mali na uwekezaji wote wa Serikali.
Aidha, itarahisisha uchambuzi wa taarifa za kifedha za Taasisi na Mashirika ya Umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Hii itawezesha Taasisi na Mashirika ya Umma kupata mrejesho wa haraka kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa maana ya maoni, mapendekezo na maelekezo kuhusiana na taarifa za kifedha zinazowasilishwa,” alisema Msajili wa Hazina.
Kuhusu kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya shajara kama wino na karatasi, Msajili wa Hazina alisema hatua hii itasaidia ofisi yake kuondokana na changamoto ya uhifadhi wa nyaraka kubwa na nyingi kutoka Taasisi na Mashirika ya Umma takriban 237 tunazozisimamia.
“Utaratibu unaotumika sasa unasababisha majalada tunayoyatumia kuhifadhi nyaraka kutoka kwenye taasisi zenu kujaa na kulazimika kufungwa ndani ya muda mfupi,” amefafanua.
Pamoja na taarifa nyingine, alisema taarifa ambazo zinaweza kuingizwa katika Mfumo wa OTRMIS kwa sasa ni za Hesabu, Utendaji wa Robo Mwaka na Taarifa za Menejimenti na wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma.
“Ni vyema tukatumbua kwamba Mfumo huu ni wetu sote na malengo ya kuanzishwa kwake ni kurahisisha utendaji kazi wa taasisi zetu. Hivyo, ni vyema mkashiriki kikamilifu na kuchangia ipasavyo ili kuwezesha Kikao Kazi hiki kuwa na manufaa kwetu sote na Taifa kwa jumla. Aidha Ofisi yetu inategemea kupata maoni na mapendekezo zaidi ya kuboresha mfumo huu kwa kadri itakavyoonekana inafaa.” alisema Msajili wa Hazina.
Benedicto pia alibainisha kuwa katika kikao kazi hicho washiriki watapatiwa pia mafunzo kuhusu uhamishaji wa vifungu vya Bajeti (Reallocation) katika Mfumo wa PLANREP ili kuwapa uelewa wa suala hilo na kuwezesha taasisi zinapokuwa na uhitaji wa uhamishaji wa vifungu vya bajeti kufanya hivyo hasa kwa kuzingatia kwamba tayari utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2021/22 umeshavuka kipindi cha miezi sita.
“Aidha, nategemea pia kwamba baada ya Kikao Kazi hiki mtakuwa mmepata uelewa wa kutosha wa namna ya kuutumia mfumo huu wa FARS na mtaenda kuwa walimu wa wenzenu kwenye taasisi mlizotoka.
“Hatutegemei kwamba Taasisi zenu zitakuwa na watumishi watatu tu waliohudhuria mafunzo haya kuwa ndio wana uelewa wa kuutumia Mfumo huu, bali watumishi wengi kwa kadiri itakavyowezekana ili kipindi ambacho hamtakuwepo kwa sababu mbalimbali kuwe na watumishi wengine watakaokuwa na uwezo wa kutumia mfumo na kuwasilisha taarifa zinazotakiwa katika Ofisi ya Msajili wa Hazina,” alisema Benedicto.
Aidha, ameagiza taasisi zote kujaza taarifa za hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2020/2021 kabla ya Machi 30, 2022.