Marekani na Japan wameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa China na kuahidi kushirikiana dhidi ya jitihada za kuidhoofisha kanda hiyo, ikiwemo kuibuka kwa vitisho vya ulinzi. 

Taarifa ya washirika hao wawili imetolewa baada ya mazungumzo kwa njia ya mtandao ya mawaziri wa mambo ya kigeni na ya ulinzi wa mataifa hayo mawili ambayo yaliangazia jinsi kitisho kinachoongezeka kuhusu China na mvutano unaoongezeka juu ya Taiwan kinavyoliweka jukumu la usalama la Japan katika umuhimu mkubwa. 

Mawaziri hao wameelezea wasiwasi kuwa juhudi za China za kuhujumu utaratibu unaozingatia sheria, zinaleta changamoto za kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiteknolojia kwa kanda hiyo na ulimwengu mzima. 

China kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni imelaani kauli hizo zilizotolewa na Marekani na Japan. Msemaji wa Wizara hiyo amesema China imewasilisha malalamiko yao kwa nchi zote mbili.