Kubanwa na mkojo
Kibofu cha mkojo hufanya kazi kwa mfumo wa kujiendesha wenyewe yaani, automatic, kitendo cha mtu kupuuzia kwenda kukojoa husababisha Ubongo upate usumbufu wa taarifa za kujaa kwa kibofu cha mkojo na kwa kuwa Ubongo nao hutuma taarifa katika kibofu cha mkojo kusema kuwa mkojo uendelee kushikiliwa mpaka muda muafaka utakapofika, itafika kipindi uwezo wa ubongo kutoa taarifa hizi na pia uwezo wa vigunduzi asili (Receptors) vilivyoko katika kibofu cha mkojo kupoteza uwezo wake tena wa kufanya kazi hizo au uwezo kuwa mdogo. 

Matokeo yake ni mtu siku kweli anahitajika kuvumilia kidogo ili afike sehemu inayostahihi kujisaidia, lakini hawezi tena na kujikuta muda mdogo tu….mtu tayari kaloanisha nguo yake.

Mpenzi msomaji, mtu kujibana na kupuuzia kwenda kukojoa husababisha uwezo wa kibofu cha mkojo kujitawala (control) upotee. Pia kama uwezo wa neva zinazopeleka taarifa kwenye ubongo kuhusu mabadiliko/ujazo wa kibofu cha mkojo zitaharibika, basi misuli maalumu ya kubana mkojo (sphincter) itashindwa kuachia na matokeo yake mtu ataendelea kukaa na mkojo katika kibofu chake kwa muda mwingi zaidi kitu ambacho ni hatari kwa afya yake. 

Endapo mkojo huu utashindwa kutoka, utatengeneza mazalia ya bakteria na kukusababishia magonjwa ya kibofu (bladder infection). Magonjwa ya kibofu cha mkojo ni pamoja na U.T.I (Urinary Tract Infections), pia huweza kusababisha magonjwa ya figo na mchafuko wa damu, bacteremia.

Kuna hali huwa inajitokeza kwa baadhi ya watu, yawezekana alikuwa kabanwa na mkojo au alikuwa hajahisi kwenda kukojoa, ila akinywa maji au akisikia sauti ya maji yanachuluzika mfano maji yakitoka bombani, basi atahisi kwenda kukojoa.

Mpenzi msomaji, ni vyema tukawa wasikivu pale mtu unapobanwa na mkojo, hii ni kwa ajili ya afya ya kibofu chako cha mkojo lakini pia ni kwa ajili ya afya yako kwa ujumla. Kama unalo tatizo, usisite kuonana na wataalamu wa afya.