Na WMJJWM-DSM
Serikali imesema Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Kati ni mojawapo ya wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyowasababishia kushuka kwa ufanisi kwenye masomo yao, hivyo kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wa mwaka 2017/18-2021/22 Serikali kwa kushirikiana na Wadau wake inatekeleza Mpango wa uanzishaji wa Madawati ya Jinsia katika Vyuo hivi ili kukomesha vitendo hivyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Dawati la Jinsia chini ya Mradi wa Our Right, Our Lives, Our Future (03 plus) unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO ) Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (Mb) alisema Madawati hayo yatasaidia kupambana na Ukatili wa Kijinsia vyuoni hivyo, yasimamiwe kikamilifu yalete tija na yasiwe ya utendaji wa mazoea.

Amesema, Serikali itasimamia kuanzia Vijijini hadi Taifa kuimarisha mifumo ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na amewaomba UNESCO kushirikiana na Serikali ili huduma hii ifike kwenye vyuo vyote 512 nchini.

“Kuna matukio mengi ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii na yanaongezeka siku hadi ikiwemo vyuoni hivyo, huu ni wakati wa kuyatokomeza kwa kuweka mikakati madhubuti ikiwemo Dawati la Jinsia kwenye kama ilivyoelekezwa na Serikali” alisema Dkt. Gwajima.

Vielvile, Dkt Gwajima amesema, Madawati hayo yanatakiwa kuwa Hai, madhubuti na yanayofanya kazi kwa vitendo wakati wote kwa kuwasaidia wahanga wa vitendo vya ukatili kwa kuwapatia huduma stahiki.

“Tutakuwa tunafanya ziara ya mara kwa mara kutembelea madawati haya pia tutakuwa na mfumo wa kupima utendaji wake ili isije ikawa tumefungua kwa mazoea yakakosa tija” alisisitiza. Dkt. Gwajima.

Hata hivyo alisema, Serikali imetekeleza mambo mengi katika kupambana na ukatili wa kijinsia mathalani kukuza uelewa wa wananchi ambapo matukio 20,025 yameripotiwa mwaka 2020/21 ikilinganishwa na 18,270 mwaka 2019/20, Madawati ya Jinsia 420 yameundwa kwenye Vituo vya Polisi na 153 kwenye Jeshi la Magereza, Kamati 18,186 za Ulinzi wa Wanawake na Watoto zimeanzishwa nchini, vituo vya huduma kwa wahanga vimeanzishwa kwenye hospitali 14, Sheria ya msaada kwa wahanga na 1 ya mwaka 2017 imetungwa na mambo mengine mengi.

Naye, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga, alisema mradi wa ‘03plus’ utanufaisha Vyuo Vikuu vya Dar Es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na juhudi zitaendelea kupanua huduma hii kwenye vyuo vingine nchini “Serikali ya awamu ya sita imejipanga kikamilifu kuondoa hii changamoto ya ukatili wa kijinsia” alisema Kipanga.

Katika uzinduzi huo Makamu Mkuu wa Chuo Profesa, William Anangisye alisema mradi wa “03plus” una malengo matatu ambayo ni kuondoa mimba za utotoni, kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi na kutokomeza kabisa ukatili wa kijinsia katika vyuo vikuu. Pia alisema mradi huo unalenga kutimiza malengo ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kati.

Aidha Mkurugenzi Mwakilishi wa UNESCO nchini Tirso Santos alisema, lengo la kuleta mradi huo ni kutaka kuona wanafunzi wa vyuo vya juu wanasoma huku wakijiamini “Wanafunzi wengi wa kike wanasoma bila ya kujiamini kwa sababu ya kupata changamoto za ukatili wa kijinsia”alisema Santos.

Wakiongea wakati wa hafla hiyo wanachuo Sauda Charled na Upendo Lugemdo, kutoka Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam na Dodoma wameipongeza Serika na Wadau kwa kushirikiana kutekeleza Mpango wa Dawati la Jinsia ambao wamesema utakuwa mkombozi kwao.