Kimbunga kikali cha msimu wa baridi Malik, kimepiga maeneo ya kaskazini mwa Ulaya na kusababisha vifo vya watu wanne.

Kimbunga hicho ambacho kimetokea wikendi hii pia kimesababisha uharibifu wa nyumba, magari na madaraja huku kikisababisha mafuriko na kusitisha usafiri.

Nchini Scotland, mama mwenye umri wa miaka 60 aliuawa pamoja na kijana mmoja baada ya kuangukiwa na miti Jumamosi, kufuatia upepo mkali wa kimbunga hicho.

Nchini Denmark vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeripoti kwamba mwanamke mwenye umri wa miaka 78 alifariki dunia kutokana na majeraha mabaya alipoanguka kutokana na upepo mkali.

Katika nchi jirani Ujerumani, vyombo vya habari nchini vimeripoti kwamba mwanamume mmoja aliuawa jana baada ya kuangukiwa na bango la biashara kufuatia upepo mkali wa kimbuka Malik.

Athari za kimbunga Malik ikiwa ni pamoja na upepo mkali na mvua nyingi, zimeendelea kushuhudiwa Jumapili katika nchi za kanda ya kaskazini ya Ulaya mfano Denmark, Finland, Norway na Sweden.