Awamu ya nne ya kura ya kumchagua rais mpya wa Italia imeshindikana baada ya muungano wa vyama vikuu vya kisiasa kuamua kutopeleka wagombea, wakati wakijaribu kukubaliana kuhusu mgombea anayekubalika na pande zote kwenye nafasi hiyo muhimu. 

Pande zote zimeonesha kuwa zinataka kuongeza kasi ya mazungumzo na waziri mkuu wa zamani, Matteo Renzi ametabiri kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa ifikapo kesho Ijumaa. 

Kinyang'anyiro cha kuwania urais kiko wazi na hakuna kambi ya chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia wala siasa za wastani za mrengo wa kushoto wana kura za kutosha katika bunge kushinikiza mgombea wao binafsi. Hatua hiyo inamaanisha makubaliano ya aina fulani yanahitajika. 

Waziri Mkuu Mario Draghi bado anasalia kuwa mgombea wa nafasi hiyo, lakini matarajio yake yamefifia wiki hii, huku wabunge wengi wakisita kumuunga mkono kwa sababu wanaogopa mabadiliko yoyote ya serikali yanaweza kusababisha uchaguzi wa mapema.