Dkt. Mollel Atinga Hospitali Ya Temeke Ateta Na Wafanyakazi, Ataka Bilioni 4.9 Za Serikali Kuboresha Huduma Za Kibingwa
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wa awamu ya Sita, Mh. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha huduma bora za kitabibu za kibingwa pamoja na miundombinu katika Hospitali zake nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Godwin Mollel ambaye aliyefanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, alipoenda kusikiliza kero na kujionea utendaji kazi wa hospitalini hapo.
Dkt. Kimaro aliwapa salamu za Rais Mh. Samia Suluhu Hassan na kuwataka waendelee kuchapa kazi kwani ameweza kupeleka fedha kiasi cha Bilioni 4.9.
Dkt. Mollel ambaye pia ni bingwa wa upasuaji ameishukuru Serikali kuwapatia fedha hizo ambazo zitakwenda kutatua changamoto nyingi inazokabiliana nazo.
Amebainisha zitakwenda kuboresha eneo la kitengo cha kuhudumia wagonjwa wa dharura {EMD}, ukarabati mkubwa wa chumba cha uangalizi maalum (ICU) pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa kwa kiasi cha Sh. bilioni 1.3.
Tutaboresha miundombinu ya uchunguzi (radiolojia), tutanunua CT Scan yenye uwezo mzuri na hivyo tutapunguza shida ya wakazi wa temeke kwenda kufuata huduma hizi nje ya hospitali,” alisema Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amesema Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ujumla Wilaya ya Temeke imepatiwa kiasi cha Sh. bilioni tisa (Bil 9) kuboresha sekta ya afya na kwamba kati ya hizo kiasi hicho cha Sh. bilioni 4.9 kimewasilishwa hospitalini hapo.
“Zimeletwa kuboresha huduma, miundombinu na kuweka vifa tiba vingine ambavyo vitawezesha kuboresha huduma za afya kwa wananchi, kiujumla nchi nzima zimepelekwa zaidi ya Sh. bilioni 495 kuboresha huduma za afya” Alieleza Dkt. Mollel.
Aliongeza kuwa, fedha hizo ni nyingi kuwahi kutokea kupelekwa eneo la afya pekee nchini na hizo ni nje ya fedha zilizopitishwa kwenye bajeti ya afya, ambapo alifafanua kuwa hizo zilipitishwa kwa namna ya dharura na Bunge.
“Ndiyo maana nimekuja na kuzungumza na timu za usimamizi wa huduma ndani ya hospitali, ngazi ya wilaya na mkoa na wafanyakazi kujadiliana na kuhimizana kuboresha huduma kwa mteja,” Alisema Dkt. Mollel.
Amesema kwa mwezi hospitali hiyo wanakusanya kiasi cha Sh. milioni 350, ikiwa watazingatia kuboresha huduma kwa mteja watavuka makusanyo hayo.
“Wakijipanga wanaweza kuzalisha zaidi ya Sh. milioni 350 kwa mwezi maana yake ifike mahala hospitali zetu ziweze kujiendesha zenyewe, ziangalie tunajipangaje tuipunguzie Serikali kuu mzigo wa kuleta hela kila mara.
Awali akiteta na wafanyakazi wa Hospitali hiyo aliweza kupokea kero na maoni zikiwemo changamoto wanazokabiriana nazo na kuahidi kwenda kuzipatia ufumbuzi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Joseph Kimaro alishukuru Serikali kwa kuwezesha kutoa fedha hizo kwani zinaenda kuongeza ubora na ufanisi wa Hospitali hiyo ikiwemo kufunga vifaa vya kisasa na kuboresha huduma na majengo.
“Tunashukuru kwa fedha hizo zitasaidia mambo mbalimbali ya uboreshaji wa huduma hapa Hospitali.
Pia kupata mashine ya kisasa ya mionzi (digital X-ray) ambayo itasaidia na x-ray nyingine zilizopo sasa.
Kwa sasa vifaa vyote hivyo vipo katika hatua tofauti tofauti za manunuzi, huku baadhi wakiwa wamesha-saini mikataba na wanatarajia kukamilisha kabla ya mwezi April, 2022 ambapo kutakuwa tayari kuna mabadiliko ndani ya hospitali hiyo.